"Jux hulipa Ksh 10K kunyolewa kichwa! - Kinyozi wa wasanii TZ

Kwa kawaida mtindo wa kunyoa wa Jux huwa shilingi 500 za Kenya lakini yeye hulipa 10K.

Muhtasari

• J4 Barbershop alisema kwamab msanii huyo huwa hahesabu pesa bali humtwanga kwa bunda la noti kuanzia 150K hadi 200K za Tanzania.

J4 na Juma Jux
Image: J4 Barbershop (Instagram)

Je, unamfahamu kinyozi ambaye anatakatisha vichwa vya wasanii wengi wa muziki kutoka nchini Tanzania?

Kama hukuwa unajua kwamba asilimia tisini ya wasanii na watu maarufu kutokea nchini Tanzania hunyolewa na kinyozi mmoja basi ndio leo utambue hilo na kulitia kibindoni.

Jamaa mmoja maarufu kwa kinyozi chake kwa jina J4 Barbershop ndiye mwenye bahati ya kuvitakatisha vichwa vya wasanii wengi tu.

Juzi kati akiwa kwenye mahojiano ya kipekee kwenye kituo cha redio cha East Africa, J4 kama anavyotambulika na wengi alipata kuzungumzia masuala mengi kuhusu kazi hiyo yake ya kurembesha vichwa vya wasanii wengi.

Pia jamaa huyo alielezea hulka za bahadhi ya wasanii ambao wanamuaminia kwa ufundi wa kuwarembesha vichwa.

Kilichoshtua wengi ni kwa jinsi alivyomzungumzia msanii maarufu na ambaye ni mwanamitindo na mwanafasheni wa kiume, Juma Jux ambaye anatambulika na wengi kutokana na uvaaji wake nadhifu na mtindo wake maarufu wa kunyoa – mtindo ambao unafanikishwa mikononi mwa J4 Barbershop.

Alisema kwamba msanii huyo mtindo wake wa kunyoa kwa wastani ni shilingi elfu 40 za Tanzania, sawa na elfu mbili pesa za Kenya lakini pindi Jux anapotimba pale na kumaliza kutakatishwa kichwa basi yeye huingia mfukoni na kutoa bunda la noti bila kuhesabu na kumpa J4.

Akielezea kiasi kikubwa ambapo aliwahi kukigundua kutoka kwa bunda hili lisilohesabiwa kutoka mifukoni mwa Jux, J4 Barbershop alisema kwamab kwa hesabu ya haraka haraka tu unaweza ukakuta Jux amekupiga kibano cha shilingi elfu mia moja na hamsini au wakati mwingine laki mbili taslimu za Tanzania ambacho ni kiasi sawa na shilingi elfu 7600 pesa za Kenya – kwa kichwa kimoja tu hicho!

Aisee kuna watu wengine huo ndio mshahara wao tena wa mwezi mzima lakini jamaa mwenye bahati anazipokea hela kiasi hicho si kwa siku moja bali kwa huduma ya kichwa kimoja tu.

J4 alizungumzia wasanii wengine ambapo alimtaja msanii Barnaba Classic kuwa msanii ambaye ana maneno mengi sana yenye ucheshi pindi anapofika kwenye kinyozi hicho.

“Wasanii wote ni wacheshi lakini Barnaba Classic kazidi akija tu huwa anatabasamu muda wote na ni mtu wa stori pia, wasanii wengine inategemea na hisia zao siku hiyo lakini kwa Barnaba yeye huwa ni mwenye tabasamu tu muda wote,” J4 huyo akizungumza kwenye mahojiano.