"Nilikosana na mke wangu juu si mfuasi wa Raila, nishauri" Mwanaume asema

Msimu huu wa siasa wanandoa wengi hukosana sababu kila mmoja anashabikia mwanasiasa anayemkubali.

Muhtasari

• Mwanasaikolojia alishauri watu kuwa katika mahusiano na watu wenye kudhibiti hisia zao hata baada ya tofauti za kisiasa.

The Star
Image: Creativemarket.com

Ni ule wakati mwingine tena wa kisiasa ambapo kawa ilivyo kawaida ya wakenya, watu wanagawanyika katika mirengo ya kisiasa huku uhasama mkali ukiibuka baina ya watu, marafiki, ndugu na jamaa.

Msimu wa kisiasa ni kile kipindi ambacho huwa kigumu sana si tu kwa wanasiasa kuhasimiana bali pia hata miongoni mwa waumini wanaoshiriki ibada dhehebu moja na kubwa zaidi tatizo hili hujipenyeza mpaka kwenye mahusiano ya ndoa.

Unapata mume na mke kila mmoja anapigia upate mrengo anaoupenda, ambalo si jambo baya kwqa sababu kuna uhuru wa kidemokrasia nchini, lakini suala hili huzua migogoro mingi sana katika boma.

Wanaume wengi huwa wanataka wake zao kuunga mkono ule mrengo ambao wao wenyewe wanaushabikia kwa dhana kwamba ukishamuoa mwakamke kwa kumlipia mahari maanake ashakuwa bidhaa chini ya umilisi wako, kwa upande mwingine wanawake huhisi wanafaa kupewa nafasi katika ndoa kuunga mkono mrengo wanaoukubali bila kushrutishwa na wanaume wao.

Tatizo kama hili tayari lishaanza kujitokeza ambapo mwanaume mmoja alimtumia ujumbe mwanasaikolojia Benjamin Zulu akimueleza kwamba hivi majuzi ametalikiana na mkewe kwa kukaidi kushabikia kinara wa muungano wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Image: Facebook

Katika picha ya mazungumzo baina ya mwanaume huyo na mkewe aliyemfukuza na ambayo yamepakiwa na mwanasaikolojia Zulu, mwanaume huyo anamwambia mkewe kwa ukakamavu mkubwa kwamba hawezi kumkubalia kukaa naye kama hawezi kumshabikia Raila.

“Basi tulia, mimi nakupenda lakini siwezi kamwe kukubalia unipotoshe… nampenda Baba (Raila) zaidi ya ninavyokupenda wewe,” ujumbe huo ulisoma.

Baadae aliamua kutafuta ushauri kwa mwanasaikolojia ambapo Benjamin Zulu alitumia kisa chake kama mfano kushauri wafuasi wake wote kwamba ni vizuri mtu kuingia katika mahusiano na mchumba ambaye ana uwezo wa kudhibiti hisia zao kwa ajili ya kulinda uchumba ama ndoa yenu kwa gharama yoyote ile.

“Chumbiana au ingia katika ndoa na mtu mwenye ukomavu wa kudhibiti hisia zake na kulinda mahusiano yenu hata kama wakati ule mnatofautiana kisiasa,” Alishauri mwanasaikolojia Zulu.