Nyota Ndogo afunguka kuhusu uhusiano wake na wazazi wa mumewe mzungu

Mwimbaji huyo ameeleza upendo mkubwa ambao familia hiyo imemuonyesha tangu alipojiunga nayo.

Muhtasari

•"Hii familia imenipokea kwa mikono miwili, ina mapenzi mengi sana kwangu. Nafurahi sana kuwa mmoja wa familia hii," Nyota Ndogo alisema.

•Aliwasherehekea wazazi wake zake  kwa  kuishi miaka 60 pamoja na kudokeza kuwa ni hatua ambayo wazaliwa wa sasa hawawezi kupiga.

Nyota Ndogo na mumewe Henning Nielsen (picha kubwa), Wazazi wakwe wa Nyota Ndogo (Picha Ndogo)
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki mkongwe kutoka Pwani Kenya Mwanaisha Abdalla  almaarufu Nyota Ndogo amewasherehekea wakwe zake wa Denmark.

Siku ya Ijumaa, baba mkwe na mama mkwe wa Nyota Ndogo waliadhimisha miaka sitini ya ndoa yao. Nyota Ndogo alitumia ukurasa wake wa Instagram kuwasherehekea wawili hao kwa hatua kubwa walizopiga pamoja.

Mwimbaji huyo alitumia fursa hiyo kueleza upendo mkubwa ambao familia hiyo imemuonyesha tangu alipojiunga nayo.

"Hii familia imenipokea kwa mikono miwili, ina mapenzi mengi sana kwangu. Nafurahi sana kuwa mmoja wa familia hii," alisema.

Aliambatanisha ujumbe wake na video iliyowaonyesha wazazi hao wa mumewe, Henning Nielsen wakisherehekea pamoja.

Aliwasherehekea wawili hao kwa  kuishi miaka 60 pamoja na kudokeza kuwa ni hatua ambayo wazaliwa wa kizazi hiki hawawezi kupiga.

"Hii miaka jamani hiki tutatoboa kweli?" alihoji.

Wafuasi wake kadhaa walijiunga naye kuwasherehekea wazazi wakwe hao wake.

Nyota Ndogo na Bw Henning Nielsen wamekuwa kwenye ndoa ya mbali kwa takriban miaka sita. Wanandoa hao wawili walifunga pingu za maisha mwezi Mei 2016 baada ya kuchumbiana kwa muda.

Mapema mwaka huu Nyota Ndogo alifichua kuwa  ilichukua mwaka mmoja kwa yeye kujibu ombi la ndoa la mumewe huyo mzungu.

"This song imeshindwa kunitoka kichwani jamani kila nikiusikiza unanikumbusha the time mume wangu aliniuluza will you marry me Mwanaisha then nikachukua mwaka mzima kumjibu but nilikua nimekufa nimeoza unajua ukijibu haraka haraka ataona unaspeed nyingi. This song inanifanya nijiskie kumpenda mume wangu zaidi," alisema mwezi Machi.

Mwaka jana, ndoa ya Nyota Ndogo ilikuwa imesambaratika baada ya mumewe kumuacha kwa mzaha aliomfanyia mnamo siku ya Fools' Day.

Bw Nielsen alimtema mwimbaji huyo kwa miezi kadhaa na hata kumblock baada ya kumdanganya kuwa alikuwa mjamzito.