"Niliteseka sana na Waafrika!" Nyota Ndogo afunguka jinsi alivyokutana na mumewe mzungu

Muhtasari

•Nyota Ndogo amesema aliishia kuchumbiana na mzungu kutoka ughaibuni baada ya kutoridhishwa na mahusiano yake na wanaume wa Kiafrika.

•Mwanamuziki huyo amedai anafahamu watu wengi ambao wamejitosa kwenye ndoa na wazungu baada ya kujuana kupitia mitandao.

Nyota Ndogo na mumewe Henning Nielsen.
Nyota Ndogo na mumewe Henning Nielsen.
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amefichua kuwa alikutana na mpenzi wake  Henning Nielsen nchini Marekani.

Nyota Ndogo amesema aliishia kuchumbiana na mzungu kutoka ughaibuni baada ya kutoridhishwa na mahusiano yake na wanaume wa Kiafrika.

Pia ameweka wazi kuwa hakujitosa kwenye mahusiano na raia huyo wa Udenmarki ili kujinufaisha kifedha ila ni kwa minajili ya kutosheleza kiu cha mahaba.

"Mimi niliteseka sana na Waafrika. Sio kuteseka umaskini lakini mapenzi. Hapa ndio nimepata mapenzi pesa mbona natafuta mwenyewe," Nyota alisema kupitia mtandao wa Facebook.

Nyota alishinikizwa kuzungumzia suala hilo kufuatia jumbe kemkem ambazo amekuwa akipokea kutoka kwa wanadada wakiomba kuunganishwa na wazungu. Pia amefichua kuwa  kuna baadhi ya wanaume ambao wamekuwa wakiomba kuunganishwa na wazungu.

Kutokana na hayo, mama huyo wa watoto wawili amewadokezea wanaotaka wapenzi wazungu kutumia mtandao fulani ambao amedai unatumika kote duniani. 

Amedai kuwa anafahamu watu wengi ambao wamejitosa kwenye ndoa na wazungu baada ya kujuana kupitia mitandao. Hata hivyo amewashauri wafuasi wake kuwa makini wanapotumia mitandao kusaka mchumba.

"Usitumane picha ya uchi. Mtu akikuitisha picha ya uchi hakutaki anataka kukukosea tu.  Ukipata mzungu amewahi kufika Kenya wachana na hio ni Ugali Omena, inakua kila kitu," Nyota aliandika.

Nyota Ndogo na Bw Neilsen wamekuwa kwa ndoa kwa takriban miaka minane. Ingawa wawili hao hawaishi pamoja, Mdenmarki huyo amekuwa akimtembelea Nyota hapa nchini mara kwa mara.

Hapo awali mwanamuziki huyo kutoka Pwani alikuwa kwenye ndoa nyingine ambayo ilikosa kufua dafu. Ana watoto wawili kutokana ndoa yake ya kwanza.