Sonko afichua jinsi alivyofanikisha mahusiano ya Karen Nyamu na Samidoh

Karen hakupinga kauli hiyo na badala yake akamuomba asifichue zaidi.

Muhtasari

•Sonko amedai kuwa  aliwaunganisha wazazi wenza hao katika hafla ya Mugithi Night iliyofanyika Dubai miaka kadhaa iliyopita.

"Mdosi malizia tu hapo usitoe video," Karen alimjibu Sonko.

Mike Sonko, Karen Nyamu, Samidoh
Image: FACEBOOK

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amedai kuwa yeye ndiye aliyemuunganisha seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu na staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Sonko amedai kuwa  aliwaunganisha wazazi wenza hao katika hafla ya Mugithi Night iliyofanyika Dubai miaka kadhaa iliyopita.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na drama tele alikuwa akitoa maoni yake chini ya chapisho  la Karen kwenye Facebook wakati alipotoa ufichuzi huo.

"Mnafaa mniitie chai. Mimi ndio nilikupea Samidoh pale Dubai nikiwa na Moses Kuria wakati wa Mugithi night," alimwambia Karen.

Karen ambaye kwa sasa ana watoto wawili pamoja na Samidoh hakupinga kauli hiyo na badala yake akamuomba asifichue zaidi.

"Mdosi malizia tu hapo usitoe video," alimjibu Sonko.

Katika mahojiano ya hapo nyuma na Radio Jambo, Karen alifunguka kuhusu kukutana kwake kwa mara ya kwanza na msanii huyo ambapo baadae alipakia video iliyoonyesha wakijivinajiri na ikikosolewa sana mtandaoni.

Wakati huo alikana kuwa kwenye mahusiano naye na kusema kuwa uhusiano wake na Samidoh haukuwa wa kimapenzi.

"Samidoh ni rafiki yangu. Nilidhani nilichapisha tu video kama vile unavyochapisha video za marafiki zako wengine. Walakini, watu walianza kutoa maoni tofauti, kama kuhusu mke wa Samidoh, na kwa hivyo niliamua kuifuta. Sikuwa na nia yoyote mbaya, tena Samidoh ni chapa yake mwenyewe, na sikutaka kuichafua. Tulikuwa Dubai ambapo Sonko na wanasiasa wengine walikuwa pia, na tulikuwa tukikaa karibu na eneo moja, na tulipanda mashua pamoja kama marafiki," alisema.

Licha ya awali kukana kuwa kwenye mahusiano wawili hao walibarikiwa na mtoto wa kiume pamoja mnamo Novemba 2020. Karen alithibitisha Samidoh kuwa baba ya mwanawe mwezi Februari mwaka jana.

Mnamo Februari 26, Karen alijifungua mtoto wake wa pili na Samidoh.

Uhusiano wa sasa wa wazazi wenza hao hata hivyo haujulikani vizuri kwani miezi ya hivi majuzi wamesalia kimya kuhusu suala hilo.