Akothee adai kufidiwa na serikali ya Migori baada ya kutumia pesa zake kukarabati barabara

Mwimbaji huyo alisema anajivunia kazi ambayo amewafanyia wakazi wa Migori.

Muhtasari

•Akothee alichapisha video iliyomuonyesha akilalamika kwa mwanakandarasi aliyepatia kazi kwa kutotengeneza barabara kwa viwango ambavyo walikubaliana.

•"Serikali ya Kaunti ya Migori inafaa kunirudishia pesa zangu mara tu bajeti ya barabara itakapokamilika," alisema.

Akothee na Gavana wa Migori Ochillo Oyacko
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE - EZEKIEL AMINGA

Mwimbaji na mjasiriamali maarufu  Akothee amependekeza kurejeshewa pesa na serikali  ya Migori baada ya kuchukua hatua ya kukarabati moja ya barabara za kaunti hiyo kutumia pesa kutoka kwa mifuko yake.

Siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watano alichapisha video iliyomuonyesha akilalamika kwa mwanakandarasi aliyepatia kazi kwa kutotengeneza barabara kwa viwango ambavyo walikubaliana.

"Acha kuwa mwanakandarasi wa aina hiyo. Hii sio kazi ya serikali, ni pesa ya mfuko wangu. Nikikupatia kandarasi, unafanya kazi," Akothee alimwambia mwanakandarasi huyo ambaye aliandamana naye kukagua barabara hiyo.

Mwanamuziki huyo alilalamika kuhusu mashimo kadhaa kwenye barabara hiyo ambayo mkandarasi hakuwa amejaza.

Katika maelezo ya video, aliweka wazi kuwa anajivunia kazi ambayo ameweza kuwafanyia wakazi wa kaunti ya Migori.

"Barabara hii ni ya serikali, imekuwa haipitiki wakati wa mvua kubwa, watu wangu wote kutoka eneo hili waliikwepa na kutafuta njia mbadala, wengine waliegesha magari na kutumia pikipiki kwenye njia mbadala," alisema.

Alijivunia kuwa sasa barabara hiyo inaweza kupitika kwa urahisi angalau na magari yanaweza kuitumia bila shida nyingi.

"Serikali ya Kaunti ya Migori inafaa kunirudishia pesa zangu mara tu bajeti ya barabara itakapokamilika," alisema.

Akothee ni miongoni mwa wasanii tajiri zaidi nchini Kenya na katika kanda ya  Afrika Mashariki kwa jumla. Ingawa thamani yake halisi haijulikani, inaaminika kuwa kufikia sasa msanii huyo huenda tayari ni Bilionea.

Mama huyo wa watoto watano tayari amejenga jumba la kifahari la mamilioni katika eneo la nyumbani kwake Rongo, kaunti ya Migori ambapo anapanga kuishi na familia yake baada ya kustaafu.