Rayvanny awalilia mashabiki wamrudishie pete yake ya thamani

Rayvanny alikuwa mmoja wa wasanii walioalikwa kuwaburudisha wageni katika hafla ya Benki ya CRDB.

Muhtasari

•Rayvanny ametoa ombi maalum kwa mtu yeyote ambaye ataokota pete hiyo kufanya mipango ya kumrejeshea huku akiahidi kutoa zawadi nono kwake 

•Hivi majuzi alifichua kwamba alilipa shilingi bilioni 1.3 za Tanzania (Ksh 68.9m) ili kutamatisha kandarasi yake na WCB.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Staa wa Bongo Raymond Shaban Mwakyusa amefichua kwamba alipoteza pete yake ya thamani wakati akitumbuiza mjini Mbagala, Tanzania.

Rayvanny alikuwa mmoja wa wasanii walioalikwa kuwaburudisha wageni katika hafla ya Benki ya CRDB siku ya Ijumaa jioni. Alipiga shoo ya kusisimua lakini katika harakati hiyo akapoteza pete yake ya thamani jukwaani.

Bosi huyo wa Next Level Music sasa ametoa ombi maalum kwa mtu yeyote ambaye ataokota pete hiyo kufanya mipango ya kumrejeshea huku akiahidi kutoa zawadi nono kwake 

"Wanangu wa Mbagala nimedondosha pete yangu leo kwenye show ya CRDB," alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Rayvanny alimtaka mtu anayeshikilia pete hiyo ambayo alionyesha wazi kuwa ni ya maana sana kwake kuiwasilisha katika ofisi za lebo yake ya NLM.

"Atakayeiokota kuna zawadi nono kwa ajili yake anaweza kuileta NLM au anicheki DM tafadhali," alisema.

Msanii huyo wa zamani wa WCB ni miongoni mwa wanamuziki wa Bongo wanaojulikana kupenda mitindo mizuri na vito vya thamani. Yeye, bosi wake wa zamani Diamond Platnumz, mwenzake wa zamani Harmonize na wengine kadhaa mara nyingi wameonekana wakijigamba na mapambo ya thamani.

Rayvanny aliondoka katika Wasafi mwaka jana baada ya kuwa chini ya usimamizi wa lebo hiyo kwa takriban miaka sita.

Wakati akitangaza kuondoka kwake, alishukuru uongozi mzima wa WCB  ukiongozwa na Diamond ambaye amekuwa mwandani wake kwa kipindi kirefu.

“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja.. Shukrani za dhati kwa familia yangu Wasafi lakini pia kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” Alisema katika video aliyopakia Instagram.

Staa huyo aliripotiwa kuondoka kwenye lebo hiyo ya Diamond ili kuangazia na kukuza lebo yake ya Next Level Music .

Hivi majuzi alifichua kwamba alilipa shilingi bilioni 1.3 za Tanzania (Ksh 68.9m) ili kutamatisha kandarasi yake na WCB.