Esther Musila azungumzia kupata watoto na mumewe Guardian Angel

Bi Musila ana watoto watatu wakubwa, wawili wa kiume na msichana mmoja.

Muhtasari

•Musila ambaye alionekana kutopenda swali aliloulizwa alijibu, "Je, hiyo inaongezaje thamani ya maisha yako??"

•Guardian Angel aliweka wazi kuwa kupata watoto sio kipaumbele kikuu katika ndoa yake na Esther Musila.

Esther Musila na Guardian Angel
Image: Guardian Angel Instagram

Mkewe mwimbaji wa nyimbo za injili Guardian Angel, Esther Musila kwa mara nyingine tena amelazimika kuzungumzia suala la iwapo wanapanga kupata watoto pamoja.

Musila ,53, na Guardian Angel ,33, walifunga pingu za maisha mapema mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa takriban mwaka mmoja. Huku wakiendelea kufurahia ndoa yao, baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakiwapa shinikizo kupata mtoto pamoja.

"Je, Unapanga kupata mimba?" shabiki mmoja alimuuliza Musila wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram siku ya Jumanne.

Musila ambaye alionekana kukerwa na swali aliloulizwa alijibu, "Je, hiyo inaongezaje thamani ya maisha yako??"

Pia alijibu vivyo hivyo wakati mtu mwingine kwa Instagram alipotaka yeye na Guardian walete mtoto wao duniani.

Bi Musila ana watoto watatu wakubwa, wawili wa kiume na msichana mmoja. 

Katika kipindi hicho cha Maswali na Majibu, Bi Musila alibainisha kwamba hawezi kuishi bila maji, chakula na mume wake. 

Mwaka jana, mwanamuziki Guardian Angel aliweka wazi kuwa kupata watoto sio kipaumbele katika ndoa yake na Esther Musila.

Katika mahojiano ya Juni, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 32 alisema nguzo kuu uhusiano wao ni mapenzi na si watoto.

Guardian Angel alisema kwamba kupata mtoto na Bi Musila ni la ziada kutoka kwa Mungu  ambayo kwake si lazima wapate.

"Nilipoingia kwenye ndoa yetu, mtoto ni nambari mbili. Akija ama akose ni sawa. Nambari moja ni upendo wetu. Mungu akitaka kutupatia bonasi ya baraka ya mtoto ni sawa. Lakini kama haipo, hiyo ni bonasi, tunafurahia na tulicho nacho. Upendo wetu ndio ninaojali," Guardian alisema katika mahojiano na Plug TV.

Mwanamuziki huyo alisema upendo wao pekee umetosha na kueleza kuwa umemletea amani kubwa moyoni.

"Tukipata mtoto ni sawa, tukikosa pia haipunguzi chochote kwa upendo wangu kwa mke wangu," Alisema.

Wawili hao walifunga ndoa mnamo Januari 4 mwaka jana katika harusi ndogo iliyohudhuriwa na familia na marafiki wa karibu. Hii ilikuwa baada ya kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa zaidi ya mwaka mmoja.