"Ningeolewa nawe tena!" Esther Musila ammiminia mahaba mazito mume wake, Guardian Angel

Musila, 53, amemwambia Guardian ,33, kuwa hana majuto yoyote kwa kuamua kuolewa naye.

Muhtasari

•Wawili hao walifunga ndoa mnamo Januari 4 mwaka jana katika harusi ndogo iliyohudhuriwa na familia na marafiki wa karibu. 

•Katika jibu lake kwa mke wake, Guardian Angel alisema, "Kukupenda ni maisha yangu Malkia wangu"

Esther Musila ,52, na mumewe Guardian Angel ,32.
Esther Musila ,52, na mumewe Guardian Angel ,32.
Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Wapenzi mashuhuri Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel na Esther Musila wameendelea kusherehekea ndoa yao, takriban mwaka mmoja baada ya kufunga pingu za maisha.

Wawili hao walifunga ndoa mnamo Januari 4 mwaka jana katika harusi ndogo iliyohudhuriwa na familia na marafiki wa karibu. Hii ilikuwa baada ya kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Musila, 53, sasa amemhakikishia mwimbaji huyo wa nyimbo za injili mwenye umri wa miaka 33 kwamba hana majuto yoyote kwa kuamua kushiriki maisha naye huku akisema kuwa anaweza kufanya hivyo tena na tena.

"Peter Omwaka, ningeolewa nawe tena," aliandika kwenye picha ya kumbukumbu ya harusi yao inayoonyesha wakiwa wamekumbatiana.

Katika jibu lake kwa mke wake, Guardian Angel alisema, "Kukupenda ni maisha yangu Malkia wangu"

Mwimbaji huyo pia alichapisha picha yake na mkewe kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha na emoji za moyo zinazoashiria mapenzi.

"Mpenzi wangu," Musila alijibu chini ya picha hiyo.

Wanandoa hao walikutana kwa mara ya kwanza mnamo Machi 13, 2020 na kadri siku zilivyosonga wakawa na urafiki mkubwa hadi kufikia hatua ya kufunga pingu za maisha  mapema mwaka jana.

Mwaka uliopita, wakati akiadhimisha siku ambayo walikutana, Bi Musila alieleza kuwa alikuja kumtambua Guardian Angel kupitia wimbo wake maarufu 'Rada'. Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alidokeza kwamba hakuwahi kufikiria urafiki wake na mwanamuziki huyo angekua kuwa ndoa.

"Muungano wetu usingetokea namna nyingine. Tulikuwa na mipango yetu lakini Mungu alitangulia mbele yetu na ameendelea kutuongoza katika safari yetu. Tazama Bwana amefanya yapi. Siku tulipokutana, sikuweza hata kufikiria jinsi urafiki wetu ungekuwa na maana kwangu na umbali ambao tumefikia," alisema.

Mwezi uliopita wakati akiadhimisha mwaka mmoja wa ndoa yao, Musila alisema kuwa katika hadithi za kimapenzi zote duniani ambazo zitasimuliwa, basi yao itakuwa hadithi ya kuyeyusha moyo wake muda wote.

“ Safari hii imekuwa nzuri, mimi bado ni mchumba wako, wewe bado ni bwana harusi wangu. Mwaka mmoja umepita lakini bado ni kama fungate...

..kila siku nakupenda zaidi ya siku iliyopita. Unafanya Mr & Mrs kuonekane rahisi sana," Musila alimwandikia mumewe.