Harusi tunayo! Wanafamilia wa Diamond waidhinisha ndoa yake na Zuchu

Diamond aliwasisimua wanafamilia baada ya kumtambulisha Zuchu kama mkewe.

Muhtasari

•Ndugu wa Diamond, Romy Jons na Esma Platnumz wamemkubali Zuchu kama shemeji wao mpya

•Rommy Jons kwa upande wake aliitakia kheri ndoa yake inayotarajiwa na kipusa huyo kutoka Zanzibar.

Zuchu na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Wanafamilia wawili wa karibu wa staa wa Bongo Diamond Platnumz wameonekana kuikubali ndoa yake na msanii wake Zuchu.

Esma Platnumz na Romy Jons ambao ni ndugu wa mwimbaji huyo mahiri wamemuidhinisha Zuchu kama shemeji wao mpya. Wawili hao waliweka wazi msimamo wao kuhusu uhusiano wa wasanii hao baada ya Zuchu kuchapisha picha zake na Diamond. 

Binti huyo wa malkia wa Mipasho, Khadija Kopa alichapisha picha nzuri zake na kuambatanisha na kipande cha wimbo wake mpya 'Utaniua'

"Tukikosa stuli ni sunna kula kwenye mkeka. Unijue vizuri nkinuna mie ndo nadeka. Usije dhani kiburi uniache nkaja kuchekwa. Baby raha ya shughuli mkunwa awe na hekaheka," aliimba katika sehemu aliyoshiriki.

Huku akitoa maoni yake chini ya chapisho hilo la Zuchu kwenye mtandao wa Instagam siku ya Ijumaa, Esma ambaye ni dada mkubwa wa Diamond alimtaja malkia huyo wa muziki wa bongofleva kama 'Bi Harusi'.

Zuchu alijibu ujumbe wa shemeji huyo wake kwa emoji za kicheko "😂😂"

Binamu yake Diamond, Rommy Jons kwa upande wake aliitakia kheri ndoa yake inayotarajiwa na kipusa huyo kutoka Zanzibar.

"Na ndoa yenu ikawe na kheri Inshallah," aliandika chini ya picha ya wapenzi hao wawili ambayo alipakia kwenye ukurasa wake.

Hivi majuzi, Diamond aliwasisimua wanafamilia wake na watu wengine wa karibu baada ya kumtambulisha Zuchu kama mke wake wakati wa karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya dada yake mkubwa Esma.

Baada ya kutoa hotuba yake kwenye karamu hiyo, bosi huyo wa WCB alimwalika Zuchu na kumtabulisha kama mwenzake.

"Sasa mwenzangu Zuhura akasema angependa sana tukuje pamoja. Sasa mimi ni shabiki wa maagizo naomba aje awasilishe," Diamond alisema huku chumba cha sherehe kikijawa na shangwe na nderemo.

Kabla ya kuondoka jukwaani na kuchukua nafasi yake, mwimbaji huyo pia alimtaja Zuchu kama  wifi wa dada yake Esma.

"Hapo ndipo tutajua kama ana mapenzi na wifi wake," alisema.

Wahudhuriaji wa karamu hiyo walionekana kufurahishwa sana na utambulisho wa Diamond kwa Zuchu, ishara ya wazi kuwa wengi wao wameidhinisha uhusiano kati ya wawili hao na wapo tayari kushuhudia ndoa.