Rayvanny adokeza kurudiana na Paula Kajala, amuonyesha mahaba mazito

Rayvanny ameonyesha waziwazi kuwa angali bado anampenda Paula Kajala.

Muhtasari

•Rayvanny alichapisha picha ya Paula na kuambatanisha na emoji za moyo wenye moto, ambazo kwa kawaida hutumika kuashiria mapenzi.

•Haya yanajiri takriban mwezi mmoja baada ya msanii huyo wa zamani wa WCB kudokeza kuwa anajuta kutengana na Paula.

katika picha ya kumbukumbu.
Rayvanny na Paula Kajala katika picha ya kumbukumbu.
Image: FACEBOOK// RAYVANNY

Staa wa Bongo Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny ameonyesha waziwazi kuwa angali bado anampenda Paula Kajala.

Usiku wa kuamkia Jumapili, Rayvanny alichapisha picha ya binti huyo wa muigizaji  Frida Kajala Masanja na chini yake kuambatanisha na emoji za moyo wenye moto, ambazo kwa kawaida hutumika kuashiria mapenzi.

"❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥,"  aliandika kwenye picha nzuri ya kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 ambayo alipakia Instagram.

Hatua hiyo inaonyesha kuwa huenda wawili hao bado wana uhusiano mzuri licha ya kudaiwa kuachana zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Baadhi wamechukulia kitendo cha Rayvanny kama dokezo kuwa wamerudiana.

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja baada ya msanii huyo wa zamani wa WCB kudokeza kuwa anajuta kutengana na Paula.

amemuonyesha mapenzi aliyekuwa mpenzi wake Paula Kajala.
Rayvanny amemuonyesha mapenzi aliyekuwa mpenzi wake Paula Kajala.
Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Mwezi uliopita, bosi huyo wa Next Level Music alichapisha picha ya kumbukumbu ya siku zake na Paula kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Rayvanny aliambatanisha picha hiyo yake na binti huyo wa muigizaji mkongwe Kajala Masanja wakiwa wameketi kwenye kiti na emoji ya uso uliofunikwa kwa kiganja cha mkono ambayo mara nyingi huashiria  kufadhaika au aibu.

Ingawa hakushiriki maelezo zaidi, emoji hiyo pengine ilikusudiwa kufupisha hisia zake za jumla kuhusu uhusiano wao uliovunjika.

Mwaka jana wakati akitumbuiza katika tamasha la Fiesta 2022 mjini Sumbawanga, Tanzania, Rayvanny alidokeza kusambaratika kwa mahusiano yake ya muda mrefu na mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20.

Alidokeza hayo wakati akitumbuiza wimbo wake 'Naogopa' ambapo aliongeza mistari kadhaa iliyosikika kama ujumbe wa kukiri.

"Mapenzi yasikuchanganye nakwambia, usije ukapata bila kama Dulla. Mapenzi usije kufananisha,  kama  vile chakula. Nilinyosha moyo Karula, nikaachana na Paula..." aliimba.

Baadaye, mwandani huyo wa Diamond Platnumz alidaiwa kuzozana na Paula, madai ambayo alipuuzilia mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Staa huyo aliweka wazi kuwa amejikita tu kwenye muziki na hakuwa na ubishi na mwanamke yeyote yule kote duniani.

Aikuwa akijibu tuhuma za kumshambulia mpenzi huyo wake wa zamani kwenye wimbo wake mpya wa 'Tusipanganie'.

"Mbona Paula hana habari nawe, wewe kutwa vijembe, vijembe.. fanya muziki," shabiki mmoja alimwambia Rayvanny chini ya video moja ambayo alichapisha kwa ajili ya kutangaza wimbo huo ambao aliomshirikisha Gnako.

Kwenye wimbo huo, msanii huyo wa zamani wa WCB alisikika kutuma ujumbe kwa mwanamke asiyetaja jina ambaye tayari ameshaachana naye, sababu tosha ya baadhi ya mashabiki kuamini kwamba alimzungumzia Paula.

Rayvanny hata hivyo katika jibu lake aliweka wazi kuwa maneno ya wimbo huo hayakumhusu yeyote bali alikuwa akifanya muziki tu..