Msamaha! Amira adokeza chimbuko la vita vyake na aliyekuwa mumewe, Jimal Rohosafi

Jimal na Amira wamekuwa wakirushiana vijembe siku za hivi majuzi.

Muhtasari

•Katika chapisho lake,  Amira alidokeza kuwa Jimal anapigana naye  kwa sababu alikataa msamaha wake mwaka jana.

•Jimal alidai kuwa Amira amejikita katika kuharibu jina lake kwa madai ya uwongo kwani ameacha kumlipa kodi ya nyumba.

Image: INSTAGRAM// AMIRA

Mfanyibiashara maarufu jijini Nairobi, Jimal ‘Marlow’ Rohosafi na aliyekuwa mke wake, Amira, wamekuwa wakirushiana vijembe katika siku za hivi majuzi.

Vita vyao vya mitandaoni vilichacha siku chache zilizopita baada ya Amira kusema anajuta kupata watoto na mwenyekiti huyo wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu jijini Nairobi akidai kuwa yeye ni mwanamume mkatili. Katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, mama huyo wa wavulana wawili alidai kuwa Jimal aliwahi kumpiga wakati akiwa mjamzito, madai ambayo Jimal alikanusha.

Katika chapisho lake la hivi punde, Amira alidokeza kuwa Jimal anapigana naye  kwa sababu alikataa msamaha wake mwaka jana.

"Ni kiulizo tu, sasa mtu akikuomba msamaha na hauna! Hiyo ni kitu ya kukasirikia mtu kweli? aliandika kwenye mtando wa Instagram.

Julai mwaka jana, Jimal alimuomba radhi mama huyo wa watoto wake wawili kwa drama nyingi alizosababisha kwenye ndoa yao mwaka 2021.

Katika ombi lake, Jimal alikiri kuwa alimkosea sana mkewe kwa kutekeleza wajibu wake wa kumlinda. Alimuomba Amira apokee ombi lake la msamaha huku akimkumbusha jinsi ambavyo wamepitia mengi pamoja.

"Ilikuwa mbaya kabisa. Huenda nilionekana kama mtu asiye na wasiwasi lakini sikuwa na la kufanya. Nilijua haikuwa sawa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya!Amira nafanya hivi kwa sababu ukosefu wa heshima pia ulikuwa mkubwa. Naomba radhi kwa kukosa heshima," Aliandika.

Katika jibu lake, Amira alisema hawezi kuuelewa msamaha wa mzazi mwenzake kwani ulifufua kumbukumbu ya siku mbaya za nyuma.

"Ombi hilo la msamaha limenirudisha katika sehemu moja ya giza ambayo nimewahi kuwa katika maisha yangu kwa sababu nimetafakari juu ya mengi yaliyotokea hadharani na nyuma ya milango iliyofungwa na imezua hisia nyingi," alijibu.

Mfanyibiashara huyo aliomba neema ya Mungu huku akitafakari suala hilo na kueleza kuwa kwa sasa amezidiwa na hisia.

"Vidonda vingine haviponi, lazima ujifunze jinsi ya kuishi navyo," Aliandika.

Kwenye mahojiano ya Jumatatu, Jimal alitupilia mbali madai kuwa aliwahi kumpiga mzazi huyo mwenzake akiwa mjamzito.

Alidai kwamba Amira hata hakuwa katika nafasi ya kubeba ujauzito katika kipindi ambacho anadai kuwa alimpiga.

"Ako na shida ya maumivu ya mgongo. Aliambiwa na daktari hawezi kubeba mimba, aache kudanganya watu. Hakuna siku tumewahi kuwa na mipango yake kupata mimb," alisema.

Jumatano hata hivyo, Amira alionyesha karatasi za hospitali na matokeo ya vipimo vya mimba kuthibitisha alikuwa mjamzito.

Wakati wa mahojiano na Mpasho, Jimal alidai kuwa mke huyo wake wa zamani amejikita katika kuharibu jina lake kwa madai ya uwongo kwani ameacha kumlipa kodi ya nyumba na kumpa pesa za matumizi.