Jimal Rohosafi afichua tatizo la kiafya linalomzuia aliyekuwa mkewe, Amira kupata mimba

"Mtu pekee ambaye amewahi kuwa na mimba yangu ni Amber Ray pekee yake," alisema.

Muhtasari

•Jimal alidai kuwa Amira hata hakuwa katika nafasi ya kuweza kubeba ujauzito katika kipindi ambacho anadai kuwa alimpiga.

•Jimal alidai kuwa tatizo hilo la mgongo ndiyo sababu ya Amira kujitosa kwenye safari ya kupunguza uzito wa mwili na hata kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya taratibu maalum.

Jimal Rohosafi na aliyekuwa mke wake Amira
Image: HISANI

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu jijini Nairobi, Jimal Marlow Rohosafi amekana madai ya aliyekuwa mke wake, Amira kwamba takriban miaka miwili iliyopita aliwahi kumpiga vibaya hadi kumfanya apoteze mimba.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Mpasho, Jimal alidai kwamba mama huyo wa watoto wake wawili hata hakuwa katika nafasi ya kuweza kubeba ujauzito katika kipindi ambacho anadai kuwa alimpiga.

Mfanyibiashara huyo mashuhuri alifichua kwamba walikuwa wamekubaliana kutopata watoto wengine kwani Amira ana tatizo la mgongo ambalo linafanya iwe ngumu kwake kubeba ujauzito.

"Ako na shida ya maumivu ya mgongo. Aliambiwa na daktari hawezi kubeba mimba, aache kudanganya watu. Hakuna siku tumewahi kuwa na mipango yake kupata mimba. Hakuna siku nishawahi ata kuota ako na mimba," alisema.

Baba huyo wa wavulana wawili alidai kuwa tatizo hilo la mgongo ndiyo sababu ya aliyekuwa mke wake kujitosa kwenye safari ya kupunguza uzito wa mwili na hata kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya taratibu maalum.

"Mtu pekee ambaye amewahi kuwa na mimba yangu ni mmoja tu na ni Amber pekee yake," alisema.

Jimal alibainisha kuwa hakuna jinsi angeweza kumpiga mama huyo wa watoto wake akiwa mjamzito, na mbele ya watu.Pia alibainisha kuwa umma ungejua kwa uhakika kama angekuwa na ujauzito kama anavyodai.

Alisema kuwa Amira amejitosa katika kuharibu jina lake kwa madai ya uwongo kwani ameacha kumlipa kodi ya nyumba.

"Niliacha kumpatia pesa ya matumizi wiki mbili zilizopita. Nilimwambia kuwa siwezi kuendelea kumpatia pesa ya matumizi kwa sababu nakaa na watoto na yeye pia anakaa na wao. Ni asilimia hamsini hamsini," alisema.

Mnamo siku ya Jumatatu, Wakati Amira akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram alimshtumu mume huyo wake wa zamani  kwa kuwa mtu mkatili.

Mama huyo wa watoto wawili alidai kwamba Jimal alimshambulia na kumpiga mara kadhaa wakati wa ndoa yao. Alidai kisa cha mwisho kilitokea katika nyumba yao mwaka wa 2021 na hata kumfanya apoteze ujauzito.

"Hilo lilikuwa tukio la hivi punde, acha nisiongee jinsi alivyokuwa akinipiga nikiwa na ujauzito wa mtoto wangu Amir wa miezi tisa... Safari hii alinipiga mbele ya watoto wangu, wazazi wake na familia yake na wakasimama pale kwa kweli wakimchochea ili anipige na hapo ndipo nilipomaliza (Mimba iliharibika)," alisema.

Mfanyibiashara huyo alisema kisa hicho kilitokea wakati wa sherehe ya harusi ya dadake Jimal iliyokuwa ikifanyika nyumbani kwao.

Aidha, alisema kwamba kabla ya kuamua kutoroka ndoa yake na Jimal, aliteseka kihisia, kimwili na hata kisaikolojia.

"Najua baadhi yenu mlikuwepo siku hiyo. Mnaweza kuja na kuthibitisha kama hii ni kweli. Laiti ningeweza kuandika kila kitu nilichopitia na mwanamume huyu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ilikuwa ni unyanyasaji wa kiakili, kimwili na kihisia," alisema.

Mama huyo wa wavulana wawili alisema kuwa Jimal ndiye mwanaume mbaya zaidi amewahi kukutana naye maishani. Alikiri chuki yake kubwa kwa mzazi huyo mwenzake na kubainisha kuwa daima hatawahi kumsamehe.

Amira alibainisha kuwa alivumilia ndoa sumu na Jimal Rohosafi kwa miaka mingi kwa ajili tu ya ustawi wa watoto wao.

"Nilikaa kwenye ndoa yenye sumu kwa sababu yao, nilishikilia ndoa ambayo tayari ilikuwa imevunjika. Alikuwa mtu mbaya zaidi ambaye nimewahi kukutana naye na ninamchukia sana, sitamsamehe kamwe, na hata kama nitakufa leo (Mungu tu anajua ni lini) nisingependa anizike au hata kuniomboleza,” alisema.

Aliweka wazi kuwa hajutii kamwe kugura ndoa hiyo na hata akasema kwamba anatamani angeondoka mapema.

"Nipo na raha mahali nilipo sasa," alisema.