Butita azungumzia mahusiano yaliovunjika na Mammito, ajuta kutopata mtoto mapema

Butita alisema hajawahi kuwa wazi kuzungumza kuhusu yaliyotokea kati yake na Mammito.

Muhtasari

•Butita alimkosoa Mammito kwa kukejeli kutengana kwao katika mahojiano mbalimbali ya awali.

•Butita alisema anatamani angepata mtoto akiwa kijana mdogo huku akibainisha kuwa umri wake umesonga sana.

Image: INSTAGRAM// EDDIE BUTITA

Mchekeshaji na mwelekezaji vichekesho maarufu Eddie Butita amebainisha kuwa kutengana kwake na aliyekuwa mpenziwe, Eunice Mammito ni suala nyeti.

Akizungumza kwenye mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni, Butita alisema hajawahi kuwa wazi kuzungumza kuhusu kile kilichotokea.

Alimkosoa mchekeshaji huyo mwenzake kwa kukejeli kutengana kwao katika mahojiano mbalimbali ya awali.

"Mimi sijawahi kuongelea mahusiano yangu na Mamitto. Nimemuona kwenye mahojiano kadhaa akizungumza kuyahusu na hata kufanya mzaha kuyahusu na nikasema kama anaona ikiwa vizuri kuongea kuyahusu kwa namna hiyo ni sawa. Lakini kwangu niliamua nitakaa mbali ikifika ni suala hili," alisema Butita.

Butita alibainisha kwamba ana mambo mengine mengi ya kuzingatia mbali na mahusiano yaliovunjika na mpenziwe huyo wa zamani.

Alipoulizwa anachokosa zaidi kuhusu Mammito, alikwepa swali hilo na kusisitiza kuwa hayuko wazi kumzungumzia.

Mammito alithibitisha kuvunjika kwa mahusiano yake na mchekeshaji huyo mwenzake mwezi Spetemba mwaka jana. Alithibitisha kwenye mahojiano ya simu na kituo kimoja cha redio cha hapa nchini akidai kuwa yuko kwenye mahusiano na kubainisha kwamba hajawahi kuwa peke yake hata siku moja.

“Ninakaa kukaa single ata siku moja? Nikiwachwa tu hivi watu wako kwa mstari," alisema.

Aliendelea kufichua kwamba mpenzi wake sio mtu mashuhuri, thibitisho wazi kuwa sio Butita

"Ni mtu asiye maarufu," alisema.

Baada ya Mammito kukosa kutambua siku ya kuzaliwa ya Butita mwezi Septemba 2021, uvumi wa kuachana kwao ulianza kuenea. Haikuwa ya kawaida kwa sababu ilikuwa siku ya kuzaliwa ya kwanza ambayo mchekeshaji huyo hakuwa amemtakia Butita heri njema hadharani tangu mwanzo wa mahusiano yao.

Siku moja baadaye, Mammito aliacha kumfuatilia Butita kwenye Instagram na kupelekea uvumi wa kutengana kuchacha. Wawili hao hata hivyo hawajawahi kuwa wazi kabisa kuhusu ambacho kiliwatenganisha.

Wakati wa mahojiano na Massawe, Butita aliweka wazi kuwa jambo analojuta sana ni kutopata watoto akiwa mdogo.

Mchekeshaji huyo alisema anatamani angepata mtoto akiwa kijana mdogo huku akibainisha kuwa umri wake umesonga sana.

"Saa hii imefika mahali naona sijui ni nani mkweli ama ni nani sio mkweli. Imefika mahali najiambia ni hatua nyingine ya maisha ya familia. Nafaa niwe na familia, nafaa kuwa na miaka kama mitatu ya kulea mtoto tena niwe naye hadi afike miaka 18. Saa hii vile vitu ni mingi nasimamisha wazo la familia kwanza," alisema.

Katika siku za hivi majuzi, mchekeshaji huyo anaaminika kuwa kwenye mahusiano na mrembo kwa jina Sadia Said.