Mkewe Samidoh azungumza kuhusu kumkubali Karen Nyamu kama mke mwenzake

Bi Edday alidokeza kwamba ndoa ya wake wengi inaweza tu kufanya kazi kuzimu.

Muhtasari

•Huku akijibu, Bi Nderitu ambaye alionekana wazi kutofurahishwa na ujumbe huo alisema, "Ndio, katika kuzimu."

•Hapo awali, Bi Edday alimuonya Samidoh kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Edday Nderitu, Karen Nyamu, Samidoh
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za Mugithi Samuel Muchoki na mkewe Edday Nderitu walisherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao mdogo hivi majuzi.

Wawili hao waliandaa karamu kubwa nyumbani kwa ajili ya kumsherehekea binti yao Neriah Wairimu akitimiza mwaka mmoja duniani.

Edday alibainisha kwamba karamu hiyo iliyohudhuriwa na wanafamilia pamoja na marafiki wa karibu wa familia ilikuwa ya kusisimua.

"Sherehe ilikuwa ya kupendeza , asante familia na marafiki kwa kujumuika nasi kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yangu ya kwanza, sherehe ilipamba moto, nguvu ilikuwa katika kiwango kingine," alisema kwenye Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha zake na familia yake ambazo zilipigwa wakati wa karamu hiyo ya Jumamosi.

Kama kawaida, wanamitandao wengi walijumuika chini ya chapisho hilo na kutoa maoni, baadhi wakizungumzia karamu huku wengine wakienda nje ya mada. Baadhi ya wanamitandao walitoa maoni kuhusu ndoa ya Samidoh.

"Ndoa ya wake wengi inafanya kazi," mtumizi mmoja wa Instagram alimwambia mama huyo wa watoto watatu.

Huku akijibu, Bi Nderitu ambaye alionekana wazi kutofurahishwa na ujumbe huo alisema, "Ndio, katika kuzimu."

Mwanamitandao mwingine alimwandikia, "Sasa umetuonyesha umekubali ndoa ya wake wengi kwa hivyo patia Karen uhuru wa kupost picha zake na Samidoh pia."

Alijibu, "Siku ya kuzaliwa ya mtoto na ndoa ya wake wengi inakujia wapi wacheni kulazimisha mambo."

Mwezi Februari, mama huyo wa watoto watatu alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Hii ilikuwa baada ya staa huyo wa Mugithi kuonekana na mzazi mwenzake, Karen Nyamu licha ya seneta huyo awali kutangaza uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.

Edday alidai kuwa mzazi mwenza wa mumewe anamzidi umri kwa miaka kumi, sababu nyingine inayofanya akatae kuwa mke mwenzake.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.

"Imekuwa miaka 15 kamili ya ndoa iliyojaa panda shuka, ilikuwa mwanzo mdogo ambapo kidogo ilikuwa ya kutosha kwetu, kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa maumivu,"