Dadake Diamond alalamika baada ya Zuchu kumpakulia miguu ya kuku

Licha ya kulalamika, mfanyibiashara huyo aliendelea kula chakula hicho hadi akamaliza.

Muhtasari

•Esma alisema dhumuni kubwa la ziara yake ilikuwa kumpongeza Zuchu kwa kununua gari mpya aina ya Range rover.

• Esma aliibua malalamishi kuwa mpenzi huyo wa zamani wa kaka yake mdogo alikuwa amempakulia miguu ya kuku.

•Huku akijitetea, Zuchu alidokeza kuwa mfanyibiashara huyo wa nguo aliomba kupikiwa miguu ya kuku kwa ugali.

Zuchu, Diamond, Esma Platnumz
Image: HISANI

Dada mkubwa wa Diamond, Esma Platnumz alimtembelea malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu siku ya Alhamisi jioni.

Esma alisema dhumuni kubwa la ziara yake hiyo ilikuwa kumpongeza msanii huyo wa WCB kwa kununua gari mpya aina ya Range rover.

"Hongera shoga wangu umeweza sana. Hongera sana mshikaji wangu. Umeweza sana. Gari kali sana," Esma alimwambia Zuchu.

Huku akimshukuru, Zuchu alikiri kwamba dada huyo wa bosi wake ndiye aliyempa msukumo wa kununua gari hilo la kifahari.

Baadaye, malkia huyo wa Bongo alimkaribisha Esma na rafiki mwingine ndani ya nyumba yake ambapo aliwapakulia vyakula alivyokuwa amewaandalia. Baada ya kupokea sahani yake,  Esma aliibua malalamishi kuwa mpenzi huyo wa zamani wa kaka yake mdogo alikuwa amempakulia miguu ya kuku.

"Yaani mimi baada ya kupanda gari jameni, Range. Mgeni nimefika hapa nimefanya kupewa mguu wa kuku. Kweli mie, wewe dada. Jamani baada ya kusema mimi naenda kupanda range yaliyonikuta ni haya," Esma alisema huku akiwa ameshika mguu wa kuku.

Huku akijitetea, Zuchu alidokeza kuwa mfanyibiashara huyo wa nguo aliomba kupikiwa miguu ya kuku kwa ugali.

Esma hata hivyo alimwambia mwimbaji huyo kuwa ni heri angeongeza vitamu vingine vitamu juu ya mlo huo.

"Ndio range nimepanda ila kweli miguu ya kuku kweli kama nina mimba ya kula miguu ya kuku," aliendelea kulalamika.

Licha ya kulalamika, mama huyo wa watoto watatu hata hivyo aliendelea kula chakula hicho hadi akamaliza.

amelalamika baada ya Zuchu kumpakulia miguu ya kuku
Esma amelalamika baada ya Zuchu kumpakulia miguu ya kuku
Image: INSTAGRAM// ESMA PLATNUMZ

Haya yanajiri takriban miezi miwili baada ya binti huyo mdogo wa gwiji wa taarab, Khadija Kopa na bosi wake Diamond kutangaza kuvunjika kwa mahusiano yao yaliyoaminika kuendelea kwa muda mrefu.

Mwezi Februari, Zuchu aliibua wasiwasi juu ya hali ya mahusiano yake kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa Snapchat.

Mwimbaji huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Mwimbaji huyo kutoka Zanzibar pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.

Baadaye, Diamond alizamia kwenye mtandao wa Instagram kuthibitisha kutengana na msanii huyo wake katika WCB.

Katika taarifa yake, bosi huyo wa WCB aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena. Alibainisha kuwa yeye na malkia huyo wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."