Dadake Diamond afunguka kukosana na wanafamilia kwa kuimba wimbo wa Harmonize

Mwezi Februari, Esma alizua gumzo baada ya kurekodi video akifurahiya wimbo wa hasidi huyo wa Diamond.

Muhtasari

•Esma Platnumz ametupilia mbali tetesi za kukosana na wanafamilia wake baada  ya kurekodi video akicheza wimbo wa Harmonize.

•Esma  ameweka wazi kwamba hakuomba msamaha kwa sababu ya video yake ila kwa ajili ya mwezi wa Ramadan.

Mama Dangote, Diamond Platnumz, Esma Platnumz
Image: INSTAGRAM// ESMA PLATNUMZ

Dadake Diamond, Esma Platnumz ametupilia mbali tetesi za kukosana na wanafamilia wake baada  ya kurekodi video akicheza wimbo wa Harmonize.

Akizungumza kwenye mahojiano na Wasafi Media, mama huyo wa watoto watatu aliweka wazi kwamba yeye kwa kawaida hucheza nyimbo za wasanii wengi wa Bongo  bila upendeleo, jambo ambalo wanafamilia wake wanafahamu.

"Huwa naimba nyimbo za Alikiba, naimba za Marioo,naimba nyimbo za Harmonize. Sijaona kitu kibaya kwetu na hamna mtu aliyenikasirikia," alisema.

Mfanyibiashara huyo wa nguo pia alizika tetesi kwamba uhusiano wake na Mama Dangote uliathirika baada ya kurekodi video hiyo.

"Mimi na familia yangu asilimia 100 tuko vizuri. Mamangu siku zote hawezi kugombana na mimi. Mimi ndiye mtoto wangu pendwa. Mimi na mama hatujawahi kukoseana, mimi na familia yangu sijawahi kuikosea," alisema.

Katikati mwa mwezi Februari, video ya Esma akifurahiya wimbo mpya wa Harmonize ‘Single Again’ iilivuma kwenye mitandao ya kijamii.

Dada mkubwa huyo wa Diamond alikuwa ndani ya  gari na mwanamke mwingine alipojirekodi akiimba sehemu ya wimbo huo uliotolewa  mnamo Siku ya Wapendanao.

“Masingle lady mmeona? Mimi kila siku niko single, sijui mwenzangu. Hadi siku ya Valentine's tupo single" alisikika akisema huku wimbo huo ukiendelea kucheza kwenye redio ya gari.

Mama huyo wa watoto watatu alionekana kuufurahia sana wimbo huo na hata alisikika akiimba pia huku wimbo ukiendelea kucheza.

"I'm single. Do you know that I'm single? I'm single again! Who knows that I'm single? Ooh yes, I'm single. Ladies I'm single again!I 'm single. Who knows I'm single?"  aliimba.

Siku kadhaa baadaye, mfanyibiashara huyo alizamia kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwaomba msamaha wanafamilia wake, hatua ambayo ilidaiwa kwamba ilitokana na video ambayo alirekodi.

Esma hata hivyo ameweka wazi kwamba hakuchukua hatua hiyo kwa sababu ya video yake ila kwa ajili ya mwezi wa Ramadan.

"Mimi sikuomba ndugu zangu msamaha. Nimeomba watu wengi, marafiki na hata wateja wangu. Nimeomba msamaha kwa sababu ya Ramadan. Mimi na ndugu zangu hatuna tatizo lolote," Esma alisema.

Hatua ya Esma ya kuimba wimbo wa Harmonize ilizua gumzo ikizingatiwa kuwa bosi huyo wa Kondegang ni hasidi nambari moja wa kaka yake, Diamond Platnumz.