Hamisa Mobetto afunguka kwa nini hataki watoto wake wafuate nyayo za Diamond

Mobetto ameweka wazi kwamba hataki watoto wake wawe wanamuziki katika siku za usoni.

Muhtasari

•Mobetto alibainisha kuwa kuna mambo mengi hasi yanayohusishwa na umaarufu ambayo hataki watoto wake wajihusishe nayo.

•Mobetto aliweka wazi kuwa angependa watoto wake wawe na maisha mazuri ya furaha na yaliyojaa amani.

Hamisa Mobetto na Diamond Platnumz
Image: HISANI

Mwanamitindo mrembo wa Tanzania, Hamisa Mobetto ameweka wazi kwamba hataki watoto wake  wawe wanamuziki katika siku za usoni.

Akizungumza kwenye mahojiano na Millard Ayo, mama huyo wa watoto wawili alibainisha kuwa kuna mambo mengi hasi yanayohusishwa na umaarufu ambayo hataki bintiye Fantasy Majizzo yake na mwanawe Dylan wajihusishe nayo.

"Sidhani hiyo ndiyo njia ningependa wachukue.Nadhani katika maisha kuna vitu vingi vya kufanya zaidi ya usanii. Singependa hivyo, sio starehe kuwa maarufu. Umaarufu una mazuri yake lakini kuna madhara pia," alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz aliweka wazi kuwa angependa watoto wake wawe na maisha mazuri ya furaha na yaliyojaa amani.

Mobetto alifichua kwamba amekuwa akiwaweka watoto wake faragha, mbali na watu wengi kama njia ya kuwalinda. Alidokeza kuwa wawili hao wana ujuzi mdogo sana kuhusu usanii wake  na umaarufu wake mkubwa.

"Mtoto wa kike alijua hivi majuzi kuwa mamake ni maarufu baada ya mwanafunzi mwenzake shuleni kumwambia aliniona kwenye YouTube. Mvulana hajui kabisa wala hafikirii, hayupo katika dunia hiyo. Watoto wangu nawatenga lakini nadhani hilo ndilo jambo bora kwao kwa sababu dunia ina mambo mengi," alisema.

Wakati huo huo, alifichua kwamba bado hakuna uhusiano wa karibu kati ya mpenziwe wa sasa  na watoto wake, jambo ambalo amependekeza mwenyewe. Aliweka wazi kuwa mpenzi wake anaheshimu uamuzi huo. 

"Watoto wangu hawajahi kuniona na mwanaume yeyote. Hawajahi kuona hata nikikumbatiwa. Hawajawahi kuona, kushuhudia wala kuhisi," alisema.

Aliongeza, "Sitaki kuwapatia watoto traumas ya kwamba leo mtu yupo na wana uhusiano mzuri naye alafu baada ya siku mbili, tatu hivi sisi tumeachana hawana uhusiano naye tena. Siwezi kuwaweka watoto wangu katika hali ambayo mimi mwenyewe sina uhakika nayo,"

Mwanamitindo huyo hata hivyo alidokeza kuwa mpenziwe amekuwa akiwanunulia watoto wake zawadi bila kukutana nao.

Aidha alifichua kuwa bintiye amekuwa akimuuliza kuhusu mume wake,swali ambalo limekuwa likimtatiza kujibu. 

Mobetto ana binti mmoja na mjasiriamali kwa Tanzania Francis Ciza Majizzo na mvulana anayeaminika kuwa mwanawe Diamond Platnumz. Walakini, kumekuwa na utata kuhusu mkubwa baba halisi wa mzaliwa huyo wa mwisho.