Hamisa Mobetto afunguka kuhusu kuolewa kwenye ndoa ya wake wengi

Mwanamitindo huyo alifichua kwamba amekuwa kwenye mahusiano ya siri kwa muda mrefu.

Muhtasari

•Mobetto aliweka wazi kwamba anaweza kukubali kuolewa kwa ndoa ya wake wengi ikiwa yeye ndiye atakuwa mke wa mwisho.

•Mobetto alisema kuwa mambo ambayo amewahi kupitia katika mahusiano yake ya zamani yalimfanya kuwa na wivu wa mapenzi

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Mwanamitindo maarufu wa Tanzania Hamisa Mobetto amedokeza kuwa hayuko tayari kuruhusu mume wake mtarajiwa kuoa mke mwingine.

Akizungumza kwenye mahojiano ya YouTube na Millard Ayo, mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kwamba anaweza kukubali kuolewa kwa ndoa ya wake wengi ikiwa yeye ndiye atakuwa mke wa mwisho.

Mobetto alifichua kuwa ana wivu mwingi sana na hawezi kuruhusu mumewe kuleta mwanamke mwingine baada yake.

"Labda tu mimi na mke mwenzangu tupendane, kusiwe na vurugu. Niko na wivu mwingi hasa nikipenda mtu," alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo, Diamond Platnumz alibainisha kuwa licha ya kuwa na wivu mwingi, yeye sio mwanamke wa kumfuatilia au kumchunguza mume wake

"Hata uache simu hapo, hata tuambiane namba siri, siwezi kushika simu yako," alisema.

Mobetto alisema kuwa mambo ambayo amewahi kupitia katika mahusiano yake ya zamani yalimfanya kuwa na wivu wa mapenzi na kuwa mtu wa kufikiria kupita kiasi inapofika katika masuala ya mahusiano.

Aidha,  alifichua kwamba amekuwa kwenye mahusiano na mwanaume asiyetambulishwa kwa muda mrefu sasa. Hata hivyo, alidokeza kwamba hana uhakika kamili iwapo mahusiano hayo yatageuka kuwa ndoa.

"Tupo, tunaheshimiana. Tuna furaha. Endapo itatokea kama Mwenyezi Mungu atakuwa amepanga  kwamba huyu wa sasa hivi ndio awe mume wangu, basi atakuwa ameniweka katika sehemu sahihi," alisema.

Mobetto alifichua kwamba bado hakuna uhusiano wa karibu kati ya mpenzi wake na watoto wake wawili, jambo ambalo amependekeza mwenyewe. Aliweka wazi kuwa mpenziwe anaheshimu uamuzi huo. 

"Watoto wangu hawajahi kuniona na mwanaume yeyote. Hawajahi kuona hata nikikumbatiwa. Hawajawahi kuona, kushuhudia wala kuhisi," alisema.

Aliongeza, "Sitaki kuwapatia watoto traumas ya kwamba leo mtu yupo na wana uhusiano mzuri naye alafu baada ya siku mbili, tatu hivi sisi tumeachana hawana uhusiano naye tena. Siwezi kuwaweka watoto wangu katika hali ambayo mimi mwenyewe sina uhakika nayo,"

Mwanamitindo huyo hata hivyo alidokeza kuwa mpenziwe amekuwa akiwanunulia watoto wake zawadi bila kukutana nao.

Aidha alifichua kuwa bintiye amekuwa akimuuliza kuhusu mume wake,swali ambalo limekuwa likimtatiza kujibu.