Thomas Partey akejeliwa kwa kukubali kukunjwa mashati na Grealish, "umeangusha Waafrika!"

Kwa jinsi mambo yalivyokuwa, Partey alichagua kuangusha Waafrika lakini asiangushe timu yake ya Arsenal kwani angejibu fuji hiyo pengine angeoneshwa kadi nyekundu.

Muhtasari

• Wengi wanafahamu kwamba mwanamume mzima wa Kiafrika hawezi kukubali kukunjwa mashati kwa jinsi hiyo tena bila kulipa kisasi.

• Hii ndio falsafa iliyowatuma wengi kuhusi kwamba Partey kutoka Ghana aliisaliti faraja ya wanaume wa Kiafrika.

Jack Grealish akimkunja mashati vikali Thomas Partey.
Jack Grealish akimkunja mashati vikali Thomas Partey.
Image: Twitter

Katikati mwa wiki hii, mechi ya kukata na shoka baina ya viongozi wawili katika jedwali la kigi kuu ya premia nchini Uingereza Arsenal na Manchester City ndio ilikuwa gumzo la mitaani.

Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa inatajwa kuwa ya kuamua ubingwa wa ligi utaenda wapi kati ya viongozi Arsenal na wapinzani wa karibu City, kulikuwa na mihemko pamoja na mbwembwe za aina yake ambapo kila mchezaji kutoka pande zote mbili alikuwa anajitoa kwa jino na ukucha kuhakikisha kwamba hakosei na kubeba lawama ya matokeo baada ya dakika tisini.

Tukio moja ambalo limebaki kuwa gumzo mitandaoni ni lile lililowahusisha viungo, Mghana Thomas Partey wa Arsenal na Muingereza Jack Grealish wa Manchester City.

 Katika picha ambazo zimeenea mitandaoni, Grealishi alionekana amemkunja mashati Partey kiasi kwamba alimkaba hadi kwenye koo huku maskini Partey akiwa amebabi katika kumuangalia kwa macho ya huruma aitegemea msamaha.

Tukio hilo limezua mjadala baadhi ya wanamitandao wa Kiafrika wakihisi kwamba Partey aliwaangusha kwani kitamaduni mwanamume mzima wa Kiafrika hawezi kubali kukunjwa mashati hivyo, kwani bora zichapwe tu!

“Partey ameangusha Waafrika kwa kukubali Grealish kumkunja mashati hivi bila kujibu mipigo,” mmoja kwa jina Albert Nat Hyde aliandika kwenye ukurasa wa Twitter.

“Partey amewaangusha Waafrika kwa kumruhusu Grealish kumnyakua hivi bila kulipiza kisasi. Huwezi kufanya hivi kwa Sadio Mane au hata Iheanacho. Partey ana kazi ya kufanya.” Mwingine alisema.

Lakini kutokana na uhalisia wa maneno na jinsi hali ilivyokuwa, Partey alionekana kuwa makini sana kutojibu fujo za Grealish kwani hakutaka kuiangusha timu yake kwa kurambishwa kadi nyekundu.

Wewe unasemaje kuhusu tukio hilo lililoshuhudiwa uwanjani Etihadi Jumatano ya Aprili 26?