Karen Nyamu azungumzia kuachwa na mpenzi wake Samidoh

Seneta huyo wa kuteuliwa alikuwa amedaiwa kutafuta kitulizo katika gym baada ya kuachwa na mpenziwe.

Muhtasari

•Seneta  wa kuteuliwa Karen Nyamu amepuuzilia mbali tetesi za kuachwa na mpenziwe Samuel Muchoki, almaarufu Samidoh.

•Seneta huyo wa UDA aliweka wazi kwamba yeye na mpenzi wake Samidoh hawatatengana hivi karibuni.

Karen Nyamu na mpenzi wake Samidoh
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa aliyezingirwa na utata mwingi, Karen Njeri Nyamu amepuuzilia mbali tetesi za kuachwa na mpenziwe Samuel Muchoki, almaarufu Samidoh.

Siku ya Jumatatu asubuhi, mama huyo wa watoto watatu alichapisha video yake akifanya mazoezi ya mwili na mtumiaji wa Facebook akamkejeli kwamba huwa anatorokea kwenye chumba cha mazoezi kila wakati anapoachwa na mpenzi wake, akipendekeza kwamba uhusiano wa seneta huyo na Samidoh ulikuwa umegonga mwamba.

“Kila time ukiachwa huwa unaenda kulilia kwa gym,” shabiki aliyetambulika kama Susan Mukami alijibu chini  ya video ya Karen Nyamu akifanya mazoezi.

Katika majibu yake, seneta huyo wa UDA aliweka wazi kuwa madai ya kuachwa na mpenzi wake yalikuwa ya uongo. Aliongeza kuwa yeye na mpenzi wake hawatatengana hivi karibuni.

“Usifurahishe roho yako hapo na uongo. Hehehe, sema ukweli wa moyo wako kwamba hatuachani, ikitaka kukata ikate hehehe,” Karen Nyamu alijibu.

Image: FACEBOOK?/ KAREN NYAMU

Haya yanajiri wakati ambapo kumekuwa na uvumi mwingi mjini kuhusu kwamba uhusiano wa seneta Nyamu na Samidoh huenda umeingia doa baada ya mwimbaji huyo wa nyimbo za Mugithi kuonekana akiwatembelea watoto wake wengine wanaoishi na aliyekuwa mke wake, Edday Nderitu nchini Marekani.

Mapema mwezi huu, Samidoh alifurahia muda na watoto wake watatu na Edday Nderitu nchini Marekani. Bi Nderitu na watoto wake wamekuwa Marekani kwa miezi kadhaa iliyopita tangu alipoachana na mwimbaji huyo wa nyimbo za Mugithi mapema mwaka jana kwa sababu ya migogoro ya ndoa.

Mapema wiki iliyopita, binti mkubwa wa Samidoh, Shirleen Muchoki alithibitisha kuwa msanii huyo maarufu wa Mugithi alikuwa pamoja nao nchini Marekani. Shirleen alithibitisha ufichuzi wa awali wa seneta Nyamu ambaye alikuwa wa kwanza kutangaza habari kuhusu ziara ya Samidoh katika moja ya posti zake.

Wakati akimjibu shabiki wake mmoja katika moja ya machapisho yake ya kwenye mtandao wa Facebook mapema mwezi huu, seneta huyo wa kuteuliwa alifichua kuwa Samidoh alienda Marekani kuwaona watoto wake. Pia alitumia fursa hiyo kubainisha wazi kwamba hakutakuwa na tatizo lolote kama mwimbaji huyo wa Mugithi ataamua kusuluhisha mambo na mke wake wa kwanza, Bi Edday Nderitu..

"Yeye (Samidoh) yuko pale tunapozungumza kuwaona watoto. Eddy pia akirudi kwa mix tumeshare miaka mingi sana kwa amani hatawahi kuwa tatizo,” Karen Nyamu alisema Ijumaa.

Zaidi ya hayo, aliweka wazi kuwa hangejiunga na Samidoh na familia yake nyingine Marekani kwa kuwa ingeharibu mambo, kinyume na matakwa yao.

Bi Nyamu na Samidoh wamekuwa wakifurahia mahaba yao kwa amani kwa miezi mingi sasa baada ya mke wa kwanza mwa mwanamuziki huyo, Edday Nderitu kuweka wazi kwamba amemtema ili awe na "mwanamke aliyemhitaji zaidi."