"Nampenda sana!" Harmonize kumaliza bifu na Diamond, ataja kwa nini anataka wawe marafiki

Konde Boy alifichua mpango wake wa kumpigia simu bosi huyo wake wa zamani katika kipindi cha siku chache zijazo.

Muhtasari

•Harmonize alikiri upendo wake mkubwa kwa bosi huyo wa WCB na kutaja sababu mbalimbali zinazomfanya atake wawe marafiki tena.

•Harmonize alikuwa amekaa katika lebo ya Diamond kwa takriban miaka minne baada ya kusainiwa mwaka 2015.

katika picha ya maktaba.
Harmonize na Diamond katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amezungumza kuhusu kumaliza bifu yake ya muda mrefu na anayedaiwa kuwa mpinzani wake mkuu Diamond Platnumz.

Akiongea wakati wa shoo yake ya Ijumaa usiku, mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ alifichua kuwa ana mpango wa kumpigia simu bosi huyo wake wa zamani katika kipindi cha siku chache zijazo ili kumaliza mzozo wao  wa miaka mingi.

“Nataka kutoa ahadi hapa kwamba wiki hii nataka kuhakikisha nampigia simu kaka yangu Diamond kwa sababu mimi niko tayari,” Harmonize aliwaambia mashabiki wake.

Konde Boy aliendelea kukiri upendo wake mkubwa kwa bosi huyo wa WCB na kutaja sababu mbalimbali zinazomfanya atake wawe marafiki tena.

“Sababu namba moja kwanini nimpigie simu, nampenda sana. Namba mbili, nyie mliunga mkono hata muziki wetu. Namba tatu, amesaidia sana kuupeleka muziki wa Tanzania kwenye kiwango cha kimataifa,” alisema.

Hili likitokea, itakuwa ni hatua kubwa katika tasnia ya bongo kwani mastaa hao wawili wa bongo fleva hawajawa na uhusiano mzuri tangu Harmonize aondoke WCB mwaka 2019. Alikuwa amekaa katika lebo hiyo ya muziki inayomilikiwa na Diamond kwa takriban miaka minne baada ya kusainiwa mwaka 2015.

Harmonize alianza kupata umaarufu baada ya kukutana na Diamond Platnumz na kusainiwa katika WCB Wasafi mwaka 2015. Uhusiano kati ya mastaa hao wawili wa bongo fleva hata hivyo uliharibika mwaka wa 2019 ambapo Harmonize allichukua hatua ya kuondoka katika lebo hiyo na kuwa msanii huru.

Mapema mwaka jana, bosi huyo wa Konde Music Worwide aliripotiwa kupiga hatua ya kutafuta huduma za mawakili kumsaidia kuishtaki lebo ya WCB inayomilikiwa na  Diamond kwa madai ya kunufaika na jasho lake.

Konde Boy alisema WCB imeshirikiana na wasambazaji wa muziki, Mziiki, kuchukua fedha zinazotokana na muziki wake akidai zilikuwa zinaenda kwenye akaunti ya lebo hiyo badala ya yake licha ya mkataba wake kusitishwa.

“Wasafi na Mziiki wameshirikiana kunichafua ila sijawakosea. Imekuwa kibarua kubwa kupata kile ambacho ni changu kutoka kwao ili niweze kulisha familia yangu kama wanavyofanya na familia zao," alisema mwezi Machi.

"Kwa nini waninyime kupata haki yangu ya Haki Miliki (IP) huku wakiendelea kukusanya pesa kutoka kwa IPs zangu kwa niaba yangu,” alihoji.

Wakati huo, wimbaji huyo wa kibao  'Single Again' alisema anakamilisha mipango na mawakili wake ili kupeleka kesi hiyo mahakamani hivi karibuni.

Pia alitoa wito kwa Waziri Msaidizi mpya wa Utamaduni na Sanaa, rapa Mwana FA, kumsaidia kutatua mzozo huo.

"Ninamtegemea atanisaidia kwa sababu nimeshindwa kukusanya mirabaha yangu ya muziki kwa miaka mitatu,” alisema.