"Watoto wa mama!" Harmonize na Diamond wavunja kimya baada ya kupatanishwa na rais Samia

Konde Boy alikiri ilikuwa ni hisia nzuri kukutana na hasidi wake wa muda mrefu, Diamond Platnumz.

Muhtasari

•Harmonize ametoa shukrani kwa rais Samia  kwa kumpa jukwaa la kukutana na bosi wake wa zamani Diamond Platnumz.

•Diamond pia alisherehekea kukutana na msanii huyo wake wa zamani na kumtambua rais kwa kuwaleta pamoja.

wamefurahia kupatanishwa na rais Samia Suluhu Hassan.
Harmonize na Diamond wamefurahia kupatanishwa na rais Samia Suluhu Hassan.
Image: HISANI

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ametoa shukrani zake kwa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kumpa jukwaa la kukutana na bosi wake wa zamani Diamond Platnumz.

Mastaa hao wawili wa bongo fleva ambao wanaaminika kuzozana kwa muda mrefu walikutana katika Ikulu ya Tanzania siku ya Jumanne jioni ambapo rais Samia alikuwa amewaalika watu mashuhuri kwa sherehe za Iftar.

Akizungumzia tukio hilo lililowakutanisha mastaa wengi wa bongo, Konde Boy alikiri ilikuwa ni hisia nzuri kukutana na Diamond Platnumz.

“Allah tunakuomba uzipokee fungu zetu , utusamehe makosa yetu kupitia neema ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Asante rais wetu kwa mualiko na kutuweka pamoja vijana wako,” Harmonize aliandika kwenye video yake akimkumbatia Diamond aliyochapisha kwenye Instagram.

Katika video hiyo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alionekana kufurahishwa sana na kuridhishwa sana huku akimkumbatia Diamond kwa nyuma.

“Ilikuwa nzuri kukutana nawe hapa Naseeb. Ramadhan Kareem,” aliandika.

Diamond pia alisherehekea kukutana na msanii huyo wake wa zamani katika WCB na kumtambua rais Samia kwa kuwaleta pamoja.

“Watoto wa mama kizimkazi,” aliandika.

Waimbaji hao wawili ambao wamekuwa wakitawala katika tasnia ya muziki wa bongo fleva kwa miaka kadhaa iliyopita wamekuwa hawana uhusiano mzuri kwa muda mrefu.

Katika sehemu ya wimbo wake 'My Way' , Konde Boy  aliweka wazi hakuwahi kutaka kugombana na Diamond ila akadai bosi huyo wake wa zamani alianza kumuoenea kijicho. Alibainisha kuwa hakuwahi kuwa na shida na watu waliojaribu kumzuia hapo awali

"Hata huyo ndugu yenu mi sikuvitaka vita. Mbona sikugombana na Madam Rita? Ni pressure ya kuhofia nampita. Akiskia nakohoa karoho kanampita," aliimba.

Aidha, staa huyo wa Bongo alibainisha kuwa hayuko kwenye ushindani na mtu yeyote licha ya mara nyingi kushindanishwa na Diamond.

"Siishi kwa matakwa mtu, siwezi mridhisha kila mtu. Eti nisifanye kitu kumuogopa. Huu muziki ni kipaji sishindani na mtu," alisema.

Pia alibainisha kuwa amejikita katika kujaribu bahati yake maishani na anawajali tu watu wake wa karibu.