Amira ajitolea kumfundisha mke wa Jimal kupika baada ya kupona kutokana na talaka

Mama huyo wa watoto wawili amebainisha kuwa kupona kutokana na talaka kumefanya ushirikiano katika uzazi kuwa bora zaidi.

Muhtasari

•Amira amesema yeye na watoto wameridhika na mambo yalivyo na amejitolea kumfundisha mke wa sasa wa Jimal jinsi ya kupika mapochopocho.

•Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wao kuonekana hadharani wakiwa pamoja kwa muda mrefu tangu walipotengana mwaka wa 2021.

walikutana hivi majuzi.
Jimal Rohosafi na aliyekuwa mke wake Amira walikutana hivi majuzi.
Image: INSTAGRAM// DJ ALLI BI

Wafanyabiashara mashuhuri wa Kenya, ambao pia ni wazazi wenza, Jimal Marlow Rohosafi na Amira hivi majuzi walikutana na kushiriki muda pamoja.

Video na picha za mkutano wa wazazi hao wa watoto wawili zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na msanii wa burudani kutoka Tanzania DJ Ally Bi almaarufu Asumanii.

Picha hizo zilizua hisia mseto kwenye mitandao ya kijamii na kumfanya Amira kueleza kuhusu madhumuni ya mkutano wao.

“Lol mshafika kwa DM haraka sana. Kwa hiyo watu watatu katika malezi,” Amira alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Mfanyibiashara huyo wa bidhaa za urembo aliendelea kuzungumzia jinsi kupona kutoka kwa utengano umerahisisha ushirikiano katika uzazi.

Alisema kuwa yeye na watoto wameridhika na jinsi mambo yalivyo na hata akajitolea kumfundisha mke wa sasa wa Jimal jinsi ya kupika mapochopocho.

"Kusema kweli, mara tu unapopona uzazi wenza unaweza kuwa mzuri sana. Pia mara tu unapokuwa na watoto, nyote mnajua kuwa mtu huyo atakuwa sehemu ya maisha yenu, na watoto wangu wana furaha na ni amani kwa njia hiyo, "alisema.

Aliongeza, "Hilo likiwa limesemwa, baba Shamir tafadhali mletee mkeo nimfunze kupika mapocho pocho."

Mkutano wa hivi majuzi kati ya wawili hao ni mara ya kwanza kwa wao kuonekana hadharani wakiwa pamoja kwa muda mrefu tangu walipotengana mwaka wa 2021.

Mwaka jana, Amira aliweka wazi kuwa ametengana rasmi na baba huyo wa watoto wake wawili na hata kuonyesha barua ya talaka.

Alibainisha kuwa hajutii kamwe kugura ndoa hiyo na hata akasema kwamba anatamani angeondoka mapema.

"Nipo na raha mahali nilipo sasa," alisema.

Wakati huo, mama huyo wa watoto wawili alimshtumu mume huyo wake wa zamani kwa kuwa na fitina ndogo ndogo  na uovu.

Alidai kwamba suala la ushirikiano katika malezi baina yao baada ya kutengana halikuwa rahisi hata kidogo wakati huo.

"Ni mbaya. Ninawapenda watoto wangu hadi kufa na kama ningekuwa na chaguo la kurudi nyuma  na kufanya maamuzi sahihi, nisingemchagua kama baba yao, kwa bahati mbaya maji uliyoyafulia nguo, hakuna budi kuyaogea," alisema.

Jimal na Amira walitengana mwaka wa 2021 baada ya mfanyibiashara huyo kumuoa mwanasosholaiti Amber Ray.

Amira pia alithibitisha kwamba alitalikiana rasmi na Jimal mwaka wa 2022 na akasema ana matumaini ya kuolewa tena siku moja.