Mvulana ama Msichana? Paula, Marioo hatimaye wafichua jinsia ya mtoto wao

Wapenzi Paula na Marioo waliandaa hafla maalum ya Baby Shower siku ya Jumatano, Aprili 17.

Muhtasari

•Wakati wa hafla hiyo, moshi wa rangi ya waridi uliibuka, kuashiria kuwa wapenzi hao wanatarajia mtoto wa kike.

•Wawili hao walitoa tangazo la kipekee la pamoja siku ya  Alhamisi wiki jana wakifichua kwamba Paula ni mjamzito.

Image: INSTAGRAM// PAULA KAJALA

Wapenzi maarufu wa Tanzania Paula Kajala na Marioo waliandaa hafla maalum ya Baby Shower siku ya Jumatano, Aprili 17.

Baadhi ya mastaa wenzao wa bongo ni miongoni mwa wageni waliojitokeza kuwaona wapenzi hao wakisherehekea ujauzito na pia wakiweka wazi jinsia ya mtoto wanayemtarajia.

Wakati wa hafla hiyo, moshi wa rangi ya waridi uliibuka, kuashiria kuwa wapenzi hao wanatarajia mtoto wa kike.

Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya wapenzi hao mashuhuri ambao wamekuwa wakichumbiana kwa takriban mwaka mmoja kufichua kwamba wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja.

Wawili hao walitoa tangazo la kipekee la pamoja siku ya  Alhamisi wiki jana wakifichua kwamba Paula ni mjamzito.

Walishiriki video nzuri iliyowaonyesha wakisoma gazeti lenye kichwa cha habari cha ‘A baby is on the way’ na pia kuonyesha tumbo la Paula lililochomoza.

“Ninatarajia mtoto na mpenzi wangu. Kuanzia mbili hadi tatu,” Paula aliandika chini ya video ambayo alichapisha kwenye Instagram.

Katika video hiyo, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 22 alionekana akiwa na ujauzito mkubwa huku yeye na mpenzi wake wakionyesha picha za kijusi kinachokua tumboni mwake.

Marioo ambaye kwa jina halisi ni Omary Mwanga pia alishiriki furaha yake ya kuwa baba hivi karibuni na akamshukuru binti wa muigizaji Kajala Masaja kwa kubeba ujauzito wake.

"Kuongeza mwanachama mpya kwenye kikosi chetu! Soon inshallah.. Najivunia wewe malkia @therealpaulahkajala Mungu akubariki wewe na familia,” Marioo alisema.

Mastaa hao wawili wa bongo walianza kuchumbiana mapema mwaka jana, ikiwa ni miezi michache tu baada ya Paula kuachana na mwimbaji Rayvanny ambaye alirudiana na mzazi mwenzake, Fahymah.