Mke wa Makokha, Purity Wambui alikuwa nani?- Maelezo yasiyojulikana sana kumhusu yaibuka

Marehemu Wambui anazikwa leo, Alhamisi, Juni 13 katika Makaburi ya Lang’ata, Nairobi.

Muhtasari

•Katika wasifu wa marehemu uliofikia Radio Jambo, ilibainika kuwa mama huyo wa watoto wanne alizaliwa Januari 21, 1976 na kuaga Juni 1, 2024.

•Baadaye alikutana na muigizaji Alphonse Makokha mwaka wa 1993 walipofunga ndoa na kupata watoto wanne pamoja.

alifiwa na mke wake Purity Wambui.
Muigizaji Alphonse Makhoha alifiwa na mke wake Purity Wambui.
Image: FACEBOOK// ONDIEK NYUK KAKWOTA

Maelezo kadhaa kuhusu marehemu Purity Wambui, mke wa muigizaji mcheshi Matayo Keya almaarufu Alphonse Makokha, yameibuka katika wasifu wake.

Marehemu Wambui anazikwa leo, Alhamisi, Juni 13 katika Makaburi ya Lang’ata, Nairobi. Alikufa mnamo Juni 1, 2024 baada ya vita vya muda mrefu na Saratani.

Katika wasifu wa marehemu uliofikia Radio Jambo, ilibainika kuwa mama huyo wa watoto wanne alizaliwa Januari 21, 1976 na kuaga Juni 1, 2024. Alikuwa na umri wa miaka 48 wakati alipokata roho.

Wasifu wa  marehemu ulizidi kufichua kuwa alikuwa binti wa marehemu John Thairu na Eunice Nyambura. Alikuwa mtoto wa tano katika familia ya ndugu saba.

Marehemu alisoma katika Shule ya Msingi ya St. Paul iliyo katika mtaa wa Mbotela, kaunti ya Nairobi kuanzia mwaka wa1983 hadi 1990.

Baadaye alikutana na muigizaji Alphonse Makokha mwaka wa 1993 walipofunga ndoa na kupata watoto wanne pamoja.

“Purity alifunga ndoa na Matayo Msagani Keya mwaka wa 1993, na walishirikiana kwa miaka mingi ya ajabu. Ndoa yao ilijaa upendo, heshima, na kusaidiana. Walibarikiwa wasichana wanne warembo; Maline, Sharlet, Shanice, na Malia Msagani,” wasifu huo ulisomeka.

Marehemu aligunduliwa na saratani ya matiti ya stegi ya nne mnamo Septemba mwaka jana baada ya kukabiliwa na maumivu ya mgongo na ya kichwa.

"Licha ya changamoto zake, aliendelea kuwa na nguvu na matumaini, akitumia wakati mwingi iwezekanavyo na wapendwa wake," ulisoma wasifu wa marehemu.

Marehemu Purity Wambui alilazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta mnamo Mei 29 na baadaye akaaga dunia Juni 1, 2024.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Tuko Kenya, Makokha alifichua baadhi ya mambo kuhusu familia yake na kuhusu marehemu mkewe.

Muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alifichua kwamba amekuwa kwenye ndoa na marehemu Wambui kwa takriban miaka 30.

Wakati huo. alikataa kutaja idadi kamili ya watoto wao lakini akadokeza kuwa ni wengi.

“Kikwetu huwa hatuhesabu watoto. Watoto ni wengi,” Makokha alisema.

Muigizaji huyo mkongwe hata hivyo alibainisha kuwa amekuwa akisaidia familia yake kila wakati.

“Kuwasupport nimewasupport kabisa. Hiyo ndiyo ukweli wa mambo. Kuwasupport nimewasupport, hakuna siku kumekuwa na shida yoyote. Wako sawa,” alisema.