"Hakuna anayenipata kama wewe!" Hamisa Mobetto amsifia mpenziwe kwa kuutunza moyo wake

Hamisa alimshukuru mpenziwe kwa kuendelea kuuponya moyo wake uliovunjwa na mwingine.

Muhtasari

•"Kwa  mwanaume anayenitengenezea sehemu yangu ambayo hakuivunja, asante kwa kuutunza moyo vizuri mpenzi," alisema.

•Hamisa alikiri mapenzi yake mazito kwa mpeziwe na kufichua kuwa yuko tayari kufunga ndoa naye.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Bila shaka, mwanamitindo na mwanamuziki maarufu wa Bongo Hamisa Mobetto amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba.

Matendo ya hivi majuzi ya mama huyo wa watoto wawili yanadhihirisha kuwa anayafurahia sana na kujivunia mahusiano yake ya sasa . Siku za hivi majuzi Hamisa amekuwa akizungumza mengi kuhusu mahusiano yake.

Katika chapisho lake la hivi punde, mwanamitindo huyo alimshukuru mpenzi wake ambaye bado hajamtambulisha hadharani kwa kuendelea kuuponya moyo wake uliovunjwa na mwingine. 

"Kwa  mwanaume anayenitengenezea sehemu yangu ambayo hakuivunja, asante kwa kuutunza moyo wangu vizuri mpenzi," alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz aliambatanisha ujumbe huo na picha yake nzuri inayomuonyesha akiwa ameshika shada la maua. Alimhakikishia mpenziwe kuwa hakuna aliye zaidi yake.

"Hakuna mtu anayenipata kama wewe!" alisema.

Takriban mwezi mmoja uliopita Hamisa alikiri mapenzi yake mazito kwa mpeziwe na kufichua kuwa yuko tayari kufunga ndoa naye.

"Hatimaye nimepata mtu. Nimepata mwanaume ambaye nahisi ni yeye nataka. Nahisi kama kwamba huyu ndiye mtu ningependa kushiriki maisha yangu yote naye," alisema kwa kujivunia na msisimko mkubwa.

Mwanamitindo huyo aligamba kwamba hatimaye amefanikiwa kumpata mwanamume anayezungumza lugha ya mapenzi sawa na yeye.

"Kila kitu ni rahisi sana, kila kitu ni sawa" alisema.

Mobetto alisema kuwa anatamani sana kuvishwa pete na mpenzi wake mpya na kuchukua majukumu ya mke.

"Nataka kuolewa naye. Nataka kuolewa na mtu wangu. Nataka kumpikia, nimuandalie nguo ili aende kazini. Je, hii ni ndoto? niamke? Ikiwa ni ndoto mtu tafadhali anichune niamke," alisema mwanamitindo huyo.

Aidha, alimsifia sana mpenzi wake mpya ambaye bado hajamtambulisha na kusema kuwa yeye ndiye mume kamili kwake.

"Ni kijana mzima. Ni mwananaume mwenye tabia njema. Ananukia vizuri. Anaongea vizuri,"alisema kwa madaha.

Mobetto alisema kuwa anasubiri kwa hamu jinsi mambo yatakavyokuwa wakati atakapokuwa kwenye ndoa na mpenziwe.

Kufikia sasa Mobetto amewahi kuwa kwenye mahusiano kadhaa na hata kupata watoto na wapenzi wake wawili wa zamani.

Mtoto wake wa kwanza, Fantasy Majizzo alizaliwa 2015 wakati alipokuwa kwenye mahusiano na Bw  Francis Ciza 'Majizo'. 

Dylan Abdul Naseeb ni mtoto wa pili wa Mobetto ambaye alizaa pamoja na staa wa Bongo Diamond Platnumz mnamo Agosti 8, 2017.