"Nataka kuolewa!" Hamisa Mobetto afunguka kwa nini anatamani ndoa na mpenziwe mpya

"Ni kijana mzima. Ni mwananaume mwenye tabia njema. Ananukia vizuri. Anaongea vizuri,"alisema kwa madaha

Muhtasari

•Mobetto alikiri mapenzi yake mazito kwa mpenzi wake mpya na kufichua kuwa yuko tayari kufunga ndoa naye.

•Aligamba kwamba hatimaye amefanikiwa kupata mwanamume anayezungumza lugha ya mapenzi sawa na yeye.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Mwanamitindo na mwimbaji mashuhuri wa Bongo Hamisa Mobetto amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba.

Katika video ya hivi majuzi aliyochapisha, mzazi mwenza huyo wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alikiri mapenzi yake mazito kwa mpenzi wake mpya na kufichua kuwa yuko tayari kufunga ndoa naye.

"Hatimaye nimepata mtu. Nimepata mwanaume ambaye nahisi ni yeye nataka. Nahisi kama kwamba huyu ndiye mtu ningependa kushiriki maisha yangu yote naye," alisema kwa kujivunia na msisimko mkubwa.

Mama huyo wa watoto wawili aligamba kwamba hatimaye amefanikiwa kupata mwanamume anayezungumza lugha ya mapenzi sawa na yeye.

"Kila kitu ni rahisi sana, kila kitu ni sawa" alisema.

Mobetto alisema kuwa anatamani sana kuvishwa pete na mpenzi wake mpya na kuchukua majukumu ya mke.

"Nataka kuolewa naye. Nataka kuolewa na mtu wangu. Nataka kumpikia, nimuandalie nguo ili aende kazini. Je, hii ni ndoto? niamke? Ikiwa ni ndoto mtu tafadhali anichune niamke," alisema mwanamitindo huyo.

Ingawa hajamtambulisha, Mobetto amemsifia sana mpenzi wake mpya na kusema kuwa yeye ndiye mume kamili kwake.

"Ni kijana mzima. Ni mwananaume mwenye tabia njema. Ananukia vizuri. Anaongea vizuri,"alisema kwa madaha.

Mobetto alisema kuwa anasubiri kwa hamu jinsi mambo yatakavyokuwa wakati atakapokuwa kwenye ndoa na mpenziwe.

Miezi michache iliyopita Mobetto alijitokeza kukanusha  madai kwamba amekuwa akimficha mpenzi wake wa sasa kwa kuhofia kupokonywa.

Katika mahojiano na waandishi wa habari , Mobetto alieleza kuwa kwa kawaida huwa hathamini kuyaanika mahusiano yake hadharani.

Alidai kuwa wakati mtu anapoamua kuanika mahusiano yake hadharani, basi yanakoma kuwa ya kibinafsi na kuwa ya umma.

"Mimi naamini kama kitu ni chako na Mungu amepanga, basi kitakufikia na hakitakuwa cha kuibiwa. Siamini kama mwanaume anaweza kuibiwa... Sio kama namficha. Mimi na yeye tuko vizuri katika mapenzi yetu. Tunakula, tunatembea pamoja, yaani tuko vizuri," alisema.

Pia alidai kuwa sio sawa kwake kuendelea kuwatambulisha wapenzi wapya kila wanapokuja katika maisha yake huku akibainisha kuwa tayari yeye ni mama wa watoto wawili wenye baba tofauti.

"Tukifika mbele huko kama Mwenyezi Mungu alimuandikia kuwa mume wangu basi huenda watu wataanza kumjua. Lakini sasa hivi kama tukiachana? nikipata mwingine tena nimtambulishe," Alisema.

Kufikia sasa Mobetto amewahi kuwa kwenye mahusiano kadhaa na hata kupata watoto na wapenzi wake wawili wa zamani.

Mtoto wake wa kwanza, Fantasy Majizzo alizaliwa 2015 wakati alipokuwa kwenye mahusiano na Bw  Francis Ciza 'Majizo'. 

Dylan Abdul Naseeb ni mtoto wa pili wa Mobetto ambaye alizaa pamoja na staa wa Bongo Diamond Platnumz mnamo Agosti 8, 2017.

Mapema mwaka huu Mobetto alidaiwa kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na rapa wa Marekani Rick Ross. Hii ni baada ya wasanii hao wawili kuonekana wakijivinjari pamoja katika kilabu cha Dubai.