"Inanihuzunisha hadi leo!" Eric Omondi afunguka alivyoshuhudia babake akimdhulumu mama yake

Muhtasari

•Eric alifichua kuwa amekuwa akipinga ukatili dhidi ya wanawake kwani akiwa mtoto aliwahi kushuhudia tukio linalomtia huzuni hadi sasa.

•Eric alifichua kuwa kumbukumbu ya kilichomtendekea mama yake ndiyo iliyomtia motisha wa kumsaidia mpenzi wake wa zamani Chantal

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji maarufu nchini Eric Omondi amelaani vikali unyanyasaji wa kinyumbani hasa  dhidi ya wanawake.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Eric alisema kwamba hakuna wakati ambapo mwanaume yeyote anapaswa kumpiga mwanamke.

Msanii huyo alifichua kuwa amekuwa akipinga ukatili dhidi ya wanawake kwani akiwa mtoto aliwahi kushuhudia tukio linalomtia huzuni hadi sasa. Alifunguka kuhusu  kumbukumbu  mbaya ambapo babake alimshambulia mama yake.

"Nilitoka shule nikapata mama yangu akitokwa na damu. Alikuwa hospitalini. Jicho lake lilikuwa limefura.Nilijisi mnyonge sana," Eric alisema.

Mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alisema tukio hilo lilikuwa la kuhuzunisha sana kwani alikuwa bado mtoto mdogo wa darasa la 6.

Baada ya kushuhudia hayo, Eric aliapa kulipiza kisasi kwa niaba ya mama yake. Hata hivyo haikufanyika kwani wazazi wote wawili walaga kabla hajatimiza.

"Nilikuwa najiambia nikiwa mkubwa siku moja nitalipiza kisasi kwa niaba ya mama yangu. Walirudiana wakawa wapenzi. Sijui kama iliwahi kutokea tena," Alisema.

Eric alifichua kuwa kumbukumbu ya kilichomtendekea mama yake ndiyo iliyomtia motisha wa kumsaidia mpenzi wake wa zamani Chantal ambaye anadaiwa kudhulumiwa na mchumba wake wa sasa Nicola Traldi.

"Chantal aliponipigia, hiyo kitu ilirudi. Nilijiambia  sasa mimi ni mwanaume anayeweza kusaidia," Alisema.

Ijumaa mchekeashaji huyo alichapisha taarifa mitandaoni  akidai kuwa Chantal alikuwa ameshambuliwa vibaya na mpenzi wake Nicola.

Eric  alidai kuwa Chantal alimpigia simu mwendo wa saa mbili asubuhi ya Ijumaa kumwarifu jinsi mpenzi wake alivyomshambulia.

"Nilipata Chantal amevunjika mguu. Alikuwa amenyongwa kwa shingo. Alikuwa ameangushwa kwa ngazi. Vitu vilikuwa vimepasuka. Ni mlinzi, majirani na caretaker ambao walimsaidia," Alidai.

Mchekeshaji huyo alidai kuwa Traldi amekuwa akimshambulia kipusa huyo mwenye asili ya Italia kwa muda mrefu.

Bw Traldi hata hivyo tayari amejitokeza kutupilia mbali madai ya kumdhulumu mpenziwe yaliyoibuliwa na Eric.