Inauma! Diana Marua afichua miguu yake iliyovimba huku siku ya kujifungua ikikaribia (+picha)

Mnamo Jumamosi Diana alitangaza kuwa ujauzito wake ulikuwa katika kipindi cha mwisho.

Muhtasari

•Mke huyo wa Bahati alichapisha video zinazoonyesha mwonekano mpya wa miguu yake na kulalamikia  hali hiyo mpya.

•Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwanavlogu huyo kudokeza kuwa siku ya kujifungua mtoto wake wa tatu imekaribia.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Siku ya Jumatatu mwanavlogu mashuhuri Diana Marua alionyesha miguu yake iliyovimba huku siku yake ya kujifungua ikiendelea kukaribia zaidi.

Kwenye Instastori zake, mke huyo wa Bahati alichapisha video zinazoonyesha mwonekano mpya wa miguu yake na kulalamikia  hali hiyo mpya.

"Safari hii inayoitwa mimba lakini😷😤!" aliandika.

Aliambatanisha chapisho hilo na wimbo wa Bien, 'Inauma' kuashiria kuwa huenda alikuwa akihisi uchungu kwenye miguu yake.

Katika video moja, mjakazi wake Irene Nekesa alionekana akipapasa miguu yake kwa kutumia kipande cha taulo ya kuogea ili kupunguza uvimbe.

Mama huyo wa watoto wawili alisikika akitoa sauti ya uchungu alipokuwa akihudumiwa na mfanyikazi huyo wake wa nyumbani. 

"Namshukuru Mungu kwa ajili yako Irene Nekesa. Asante kwa kunitunza katika kipindi chote hiki," Diana aliandika chini ya video hiyo.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwanavlogu huyo kudokeza kuwa siku ya kujifungua mtoto wake wa tatu imekaribia.

Siku ya Jumamosi, mke huyo wa mwanamuziki Bahati alitangaza kuwa ujauzito wake ulikuwa katika kipindi cha mwisho.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Diana alichapisha picha zake mbili, moja ya wakati hakuwa mjamzito na ya hivi punde akiwa na ujauzito uliokomaa  kisha kuchambua mabadiliko katika mwili wake.

"Imekuwa safari kubwa, kuna wakati maisha yalikuwa rahisi, wakati sikuthamini jinsi pua yangu ilivyokuwa ndogo, wakati nilitembea moja kwa moja na sio kama pengwini," alisema chini ya picha alizopakia.

Mama huyo wa watoto wawili alidokeza kuwa safari ya ujauzito wake wa tatu haijakuwa rahisi na amepitia changamoto chungu nzima.

"Kuna wakati kuamka kitandani haikuwa kazi ngumu, niliweza kulala kwa nafasi yoyote, nakosa kulala juu ya tumbo langu.

Kuna wakati niliweza kutoshea saizi ya kiatu changu bila shida yoyote. Miguu yangu sasa inashindana na ile ya tembo," alisema.

Pia alibainisha kuwa sasa hawezi kuwa bafuni kwa muda mrefu na kuoga kwa muda mrefu kwa sababu hataki tena maji ya moto.

Katika chapisho lake mtumbuizaji huyo alidokeza kuwa tayari uchungu wa leba umeanza, ishara kuwa yupo karibu kujifungua.

"Nitazungumzia jinsi mimba hii imenionyesha vumbi. Kwa sasa, nadhani nina vipindi vya mnyweo wa braxton hicks, nina maumivu," alisema.

"Acha nishughulike, nitarudi na mtoto," aliongeza na kuwasihi wanamitandao kumkumbuka katika maombi yao.