Jamaa Mtanzania ataka kununua gari, mapochopocho baada ya kulipwa Sh2000 za Kenya

Shilingi elfu mbili za Kenya ni takriban 38, 000 za Tanzania.

Muhtasari

•Alisema wakati atakapofika Dar es Salaam ataingia kwenye chumba cha maonyesho na kununua gari aina ya Mercedes Benz anayoipenda.

•Jamaa huyo alisema kuwa angetumia salio kununua pipi na kugawa miongoni mwa wakazi wa nyumbani kwake.

Image: TIKTOK// WYSE TZ

Jamaa mmoja kutoka Tanzania alijawa na bashasha isiyoelezeka baada ya kuchapa kazi nchini Kenya na kulipwa Ksh 2000.

Kijana huyo hakuweza kuficha furaha yake alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari kuhusu mipango yake na hela hizo.

"Hela kweli ninayo.Niko na elfu mbili ya Kenya. Hii siitumi mpaka nifike Tanzania, Dar es Salaam pale ,"  jamaa huyo alimwambia Wyse.

Alisema wakati atakapofika Dar es Salaam ataingia kwenye chumba cha maonyesho na kununua gari aina ya Mercedes Benz anayoipenda.

"Kutoka hapo naingia Mlimani City KFC pale. Nanunua mabawa vipapatilo themanini, mapaja hamsini nagawa Milimani nzima," alisema.

Aliongeza "Alafu pale pembeni wanauza Pepsi tamu nanunua nagawa Mlimani nzima."

Mwanamume huyo ambaye hakufichua kazi aliyofanya nchini Kenya ili kumpatia shilingi 2000 alisema kuwa angetumia salio kununua pipi na kugawa miongoni mwa wakazi wa nyumbani kwake.

Shilingi elfu mbili za Kenya ni takriban 38, 000 za Tanzania. Ni wazi kuwa kiasi hicho hakitoshi kununua baiskeli achilia mbali gari.

Jamaa huyo kutoka Tanzania hata hivyo anatumai kutumia fedha hizo zake alizozipata kwa bidii ili kutimiza haja ya moyo wake, Mungu pekee na pengine yeye anayejua jinsi atakavyofanikisha hilo.