Je, Akothee 'aliiba' mume wa mwanadada Mkenya? - Mpenziwe hatimaye avunja kimya

"Sikujali hali yake wala yeye ni nani, nilipenda sana akili yake, roho, haiba yake, nguvu na ni mrembo," alisema.

Muhtasari

•Bw Omosh amekanusha madai kwamba mwanamke huyo aliyetambulishwa kama Lucy alimuunganisha na mchumba wake Akothee .

•Bw Omosh alisema baada ya kukutana na Akothee nchini Uswizi mnamo Julai 16 kupitia rafiki yake Pius, alimpenda mara moja.

Akothee na mpenzi wake Omosh
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mpenzi wa Akothee  'Bw Omosh' amejitokeza kuzungumzia tetesi kuwa alinyakuliwa kutoka kwa mwanamke mwingine Mkenya.

Ripoti ambazo zimekuwa zikienea kwenye mitandao ya kijamii zinadai kuwa hapo awali mzungu huyo kutoka Uswisi alikuwa akichumbiana na mwanadada  mmoja wa Mombasa ambaye alimuunganisha na Akothee kabla ya hatimaye  kumwacha na kujitosa kwenye mahusiano na mwimbaji huyo.

Bw Omosh hata hivyo amekanusha madai kwamba mwanamke huyo aliyetambulishwa kama Lucy alimuunganisha na mchumba wake Akothee na kuweka wazi kuwa ni rafiki yake ndiye  aliyewaunganisha.

"Siku ya kwanza kujuana na Esther, nilikutana naye kupitia kwa rafiki yangu Pius anayeishi karibu na ziwa Zug, alikuwa Ufaransa akielekea Italia kwa likizo yake na baada ya simu hii ya video nikajiambia ni lazima nionane naye ana kwa ana," Omosh alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Bw Omosh alisema baada ya kukutana na Akothee nchini Uswizi mnamo Julai 16 kupitia rafiki yake Pius, alimpenda mara moja.

"Sikujali hali yake wala yeye ni nani, nilipenda sana akili yake, roho, haiba yake, nguvu na ni mrembo," alisema.

Amesema mwanadada anayedai kuwa mpenzi wake wa zamani alikuwa ni mshirika tu ambaye alikuwa akimsaidia kufanya ziara zake za Kenya na kuweka wazi kuwa hakuhusika kwa njia yoyote katika kukutana kwake na Akothee.

"Nilikutana na Esther bila hatia na sikuunganishwa na mwanamke kutoka Kenya. Nilimwambia Lucy kwamba rafiki yangu ana mawasiliano na mwanamke anayefanya biashara ya safari na kwamba nitakutana naye. Kisha akakumbuka kumuona katika Hoteli ya Serena Mombasa katika kiamsha kinywa muda uliopita. Lucy sio yeye aliyeunganishwa. Ilikuwa ni rafiki yangu Pius," alisema Bw Omosh.

Bw Omosh amesema alikatiza uhusiano wake na Lucy baada ya kukutana na Akothee kwani hakuhitaji huduma zake tena.

Sasa ametoa wito kwa mwanadada huyo kumwacha yeye na Akothee na kuwapatia nafasi ya kufurahia mahusiano yao kwa amani.