Karen Nyamu afichua kwa nini hawezi kushiriki katika video za muziki za mpenzi wake Samidoh

Seneta Nyamu amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Samidoh kwa takriban miaka 5 iliyopita.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa yeye na mwimbaji huyo wa Mugithi hawa hawachanganyi mahusiano yao na kazi.

•Jumatatu, Samidoh kwa mara ya kwanza alimposti seneta Nyamu na kumsherehekea vizuri kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amedokeza kuwa huenda asiwahi kuonekana katika video zozote za muziki za mpenzi wake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Wakati akiongea katika mahojiano ya hivi majuzi, mama huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa yeye na mwimbaji huyo wa Mugithi huwa hawachanganyi mahusiano yao na kazi.

"Hizo ni kazi. Hatuchanganyi kazi na mapenzi,” Karen Nyamu alisema wakati wa mahojiano kwenye YouTube channel ya Convo.

Aliongeza, "Hiyo ni kazi, iko serious!"

Mwanasiasa huyo wa UDA amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Samidoh kwa takriban miaka mitano iliyopita na wawili hao hata wana watoto wawili pamoja.

Licha ya seneta Nyamu kuyasherehekea mapenzi yao hadharani mara nyingi, mwimbaji huyo wa Mugithi amekuwa makini sana na mara nyingi ameepuka kumzungumzia hadharani, katika nyimbo zake, au hata kumposti kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Siku ya Jumatatu jioni hata hivyo, Samidoh kwa mara ya kwanza alimposti mpenzi huyo wake  na kumsherehekea vizuri kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mwimbaji huyo mashuhuri ambaye kwa muda mrefu amejaribu kuficha mahusiano hayo kutoka kwa umma aliamua kumsherehekea hadharani mama huyo wa watoto wake wawili mnamo siku yake maalum. Nyamu alikuwa anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Katika ujumbe wake kwa mpenziwe, Samidoh alimtambulisha kama ‘pacha’ wake na kukiri kwamba seneta huyo ndiye ‘scorpio’ anayempenda zaidi (mtu aliyezaliwa kati ya Oktoba na Novemba).

"Mtu tunayefanana, scorpio kipenzi," Samidoh aliandika kwenye picha yake na seneta Nyamu.

Mwimbaji huyo aliendelea kuweka wazi kwamba alikuwa tayari kutoficha uhusiano wao tena.

"Sitacheza salama. Heri ya kuzaliwa @senatorKarenNyamu,” aliandika.

Samidoh pia alitumia moja ya nyimbo zake za mapenzi kutuma ujumbe maalum kwa mama huyo wa watoto wake wawili.

Alitumia wimbo wake maarufu ‘Mumbi’ kufufua kumbukumbu ya wakati uhusiano wake ulipoanzishwa, wakati mpenziwe alikuwa na haya sana akizungumza naye. Katika wimbo huo, alibainisha kuwa hata wakati huo, angeona mustakabali machoni mwa mpenzi wake.

“Sijawahi kusahau nilipokuwa nikizungumza na wewe na ulikuwa unatengeneza michoro chini huku macho yako yakiwa yamejawa na aibu. Na nilipotazama machoni pako, ningeona mustakabali,” Samidoh alisema kwenye wimbo huo.

Chapisho la Samidoh la siku ya Jumatatu kumsherehekea mzazi mwenzake lilikuwa muhimu sana na la kipekee kwani ni nadra sana kwa mwanamuziki huyo mahiri kumpost seneta huyo au kuzungumza waziwazi kuhusu uhusiano wao hadharani.