Karen Nyamu avunja kimya baada ya mpenzi wake Samidoh kudaiwa kuongeza mke wa tatu

Tetesi hizo zilianza baada ya mwimbaji huyo kuonekana akijivinjari na kipusa mwingine ndani ya gari.

Muhtasari

•Baadhi ya wanamitandao walichukua hatua kumuuliza seneta Karen Nyamu kuhusu suala la mpenziwe kuwa na mpenzi mwingine.

•Karen alidokeza kuwa mwanamke ambaye alionekana kwenye video akiwa na mzazi huyo mwenzake si mpenzi wake bali ni shabiki tu aliyerekodi kumbukumbu naye.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: HISANI

Katika siku kadhaa ambazo zimepita, kumekuwa na uvumi kwamba staa wa Mugithi, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh yupo kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanamke mwingine, mpenzi wake wa tatu sasa.

Tetesi hizo zilianza wiki jana baada ya video ya mwimbaji huyo akijivinjari na kipusa mwingine ndani ya gari kuvuma.

Kama kawaida, watumiaji wa mtandao wadadisi walikuwa na hamu ya kujua ukweli zaidi kuhusu hilo. Baadhi hata walichukua hatua kumuuliza mmoja wa mama watoto wa Samidoh, seneta Karen Nyamu kuhusu hilo.

"Tumeskia mko watatu," mtumizi mmoja wa mtandao wa Instagram alimuuliza chini ya chapisho lake la hivi majuzi.

Karen alijibu, "Hehe, unatamani."

Mtumizi mwingine alimuuliza, "Naona bado timu inaongezeka karibu mfike timu ya mpira sasa. Unasemaje mhesh?"

Huku akimjibu shabiki huyo, seneta huyo wa kuteuliwa alidokeza kuwa mwanamke ambaye alionekana kwenye video akiwa na mzazi huyo mwenzake si mpenzi wake bali ni shabiki tu aliyerekodi kumbukumbu naye.

"Hata wewe pigwa selfie uingie," Karen alijibu.

Video iliyochapishwa kwenye chaneli ya BNN ya mwablogu Edgar Obares ilimuonyesha msanii huyo akiwa ameegemea bega kwa bega na mwanawake asiyejulikana huku akimweleza jinsi alivyo mrembo. Samidoh alionekana akitabasamu sana na kutazama kwenye kamera ambayo mwanadada huyo alikuwa ameshikilia.

Video hiyo isiyojulikana wakati ilipigwa ilionyesha mwanamke huyo aliyevalia miwani ya rangi ya kahawia akizungumza na mwanamuziki huyo kwa lugha ya Kikuyu huku akimjibu kwa maneno mazuri ya kukubaliana naye.

Samidoh alisikika akimwambia mwanadada huyo kwamba ana uwezo wa kutosha wa kuzaa watoto huku akicheka.

"Umekusudiwa kuzaa" alimwambia kwa Kikuyu.

Kisha alimuelezea jinsi wanavyofanana na kumfanya ajawe na haya usoni.

"Nitwahanana," anasema. (Tumefanana)

Jibu la mwanamke hata hivyo halikusika vizuri.

Mke wa kwanza wa mwimbaji huyo wa Mugithi, Edday Nderitu amekuwa akipinga suala la mume wake kuwa na wake wengi.

Takriban miezi miwili iliyopita, Edday alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kwamba hayuko tayari kamwe kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Hii ilikuwa baada ya mwanamuzikik huyo kuonekana na Nyamu licha ya seneta huyo awali kudai uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," Edday alimwambia mwanamuziki huyo mwezi Februari.