Karen Nyamu atumbuiza wageni kwa niaba ya mpenziwe, Samidoh kwenye harusi ya Akothee

Aliimba wimbo wa Samidoh akimshirikisha Joyce Wamama, 'Wendo wi Cama' (Mapenzi ni matamu).

Muhtasari

•Mmoja wa wageni mashuhuri kwenye harusi hiyo iliyopigiwa debe sana ni seneta wa kuteuliwa, Karen Nyamu.

•Wageni walifurahia kutumbuizwa na mama huyo wa watoto watatu huku Akothee na mumewe mpya wakicheza pamoja naye.

kwenye harusi ya Akothee mnamo Aprili 10, 2023.
Karen Nyamu kwenye harusi ya Akothee mnamo Aprili 10, 2023.
Image: HISANI

Siku ya Jumatatu, mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Omosh walifunga pingu za maisha kwenye harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, Nairobi.

Harusi ya pili ya mwimbaji huyo ambayo ilifanyika mnamo siku yake ya kuzaliwa ya 43 ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii maarufu na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua 300 walikuwa wamealikwa.

Mmoja wa wageni mashuhuri kwenye harusi hiyo iliyopigiwa debe sana ni seneta wa kuteuliwa, Karen Nyamu.

"Niko hapa kwa siku kuu ya Akoth. Hongera mama! Mapenzi ni kitu kizuri @akotheekenya," Nyamu alisema.

Huku harusi ikiendelea, seneta huyo wa UDA alionekana akiimba, kucheza na kutangamana  na wageni wengine kwa furaha tele.

Wakati fulani, Karen alisimama kwenye jukwaa, akapewa kipaza sauti na kuwatumbuiza wageni kwa wimbo. Aliimba  wimbo wa mpenzi wake Samidoh akimshirikisha Joyce Wamama, 'Wendo wi Cama' (Mapenzi ni matamu).

Wageni walifurahia kutumbuizwa na mama huyo wa watoto watatu huku Akothee na mumewe mpya wakicheza pamoja naye.

"Asante, asante sana," Karen alisema baada ya kutumbuiza.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya seneta huyo kuchukua hatua kubwa ya kubadilisha picha yake ya wasifu kwenye  Instagram na kuweka picha inayomuonyesha akiwa na mzazi mwenzake, Samidoh pamoja na binti yao mdogo.

Nyamu alitumia moja ya picha  walizopigwa wakati wa kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yao Wairimu mwezi Februari mwaka huu.

Wakili huyo amekuwa akikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na uhusiano wake wa muda mrefu na Samidoh. Wawili hao wamekuwa mahusiano yaliyojaa drama kemkem kwa muda na hata wamebarikiwa na watoto wawili pamoja.

Mwezi Februari, mkewe Samidoh, Bi Edday Nderitu alimwandikia ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Hii ilikuwa baada ya staa huyo wa Mugithi kuonekana na Karen Nyamu licha ya seneta huyo awali kutangaza uhusiano wao umefika mwisho. Edday alibainisha kwamba hayuko tayari kumkubali Nyamu kama mke mwenzake.