"Huyu ndiye anabamba!" Seneta Karen Nyamu ajivunia kuwa mke wa pili wa Samidoh

Karen na Samidoh wamekuwa wakichumbiana kwa muda na wana watoto wawili pamoja.

Muhtasari

•Baadhi ya wanamitandao walimsihi wakili huyo kumuiga Akothee na kufanya harusi hivi karibuni pia.

•Wakati wa harusi ya Akothee, Nyamu aliimba  wimbo wa Samidoh akimshirikisha Joyce Wamama, 'Wendo wi Cama' (Mapenzi ni matamu).

Karen Nyamu, Samidoh, Edday Nderitu
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu ni miongoni mwa makumi ya watu mashuhuri waliohudhuria harusi ya Akothee siku ya Jumatatu.

Mnamo siku hiyo, mama huyo wa watoto watatu alimpongeza mwanamuziki huyo kwa hatua kubwa ya maisha ambayo alipiga.

"Niko hapa kwa siku kubwa ya Akoth. Hongera mama! Mapenzi ni kitu kizuri," Nyamu alimwambia Akothee kwenye Instagram.

Kama kawaida, wanamitandao walipiga kambi kwenye chapisho la seneta huyo wakitoa aina tofauti za maoni. Baadhi walizungumzia maneno kwenye chapisho hilo kuhusu huku wengine wakitoka nje ya mada.

Baadhi ya wanamitandao walitumia fursa hiyo kumsihi wakili huyo kumuiga Akothee na kufanya harusi hivi karibuni pia.

"Tafuta wako sasa pia wewe ufanye harusi," mtumizi mmoja wa mtandao wa Instagram alimwambia seneta huyo.

Karen alijibu, "Nitafanya na wenyu."

Mtumizi mwingine wa Instagram alimtaka mama huyo wa watoto watatu aachane na mume wa mtu mwingine na atafute wa kwake.

"Tafuta wako sasa sio ya wenyewe," maggy9246 aliandika.

Wakili huyo alijibu, "Huyu ndio anabamba."

Wakati wa harusi ya Akothee, seneta huyo alionekana akiimba, kucheza na kutangamana  na wageni wengine kwa furaha tele.

Kwa wakati fulani, alisimama kwenye jukwaa, akapewa kipaza sauti na kuwatumbuiza wageni kwa wimbo. Aliimba  wimbo wa mpenzi wake Samidoh akimshirikisha Joyce Wamama, 'Wendo wi Cama' (Mapenzi ni matamu).

Wageni walifurahia kutumbuizwa na mama huyo wa watoto watatu huku Akothee na mumewe mpya wakicheza pamoja naye.

"Asante, asante sana," Karen alisema baada ya kutumbuiza.

Takriban miezi miwili iliyopita, mkewe Samidoh, Edday Nderitu alimwandikia ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Hii ilikuwa baada ya staa huyo wa Mugithi kuonekana na Nyamu licha ya seneta huyo awali kudai uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," Edday alimwambia mwanamuziki huyo mwezi Februari.

Edday alisema ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita