Kweli wametengana? Wasiwasi waibuka kuhusu ndoa ya Harmonize na Kajala

Maswali kuhusu iwapo Harmonize na Kajala bado wako pamoja yameibuka.

Muhtasari

•Matukio ya hivi majuzi  yamezua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wao ambao wamekuwa wakihoji kuhusu kinachoendelea ndani ya mahusiano yao.

•Imebainika kuwa amebalisha bio yake ya Instagram kutoka 'mke wa @harmonize_tz' na kusalia kuwa Mama ya @therealpaulahkajala na mke na meneja.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE, KAJALA MASANJA

Maswali kuhusu iwapo bosi wa Konde Music Worldwide Harmonize na muigizaji Fridah Kajala Masanja bado wako pamoja yameibuka.

Matendo ya katika siku za hivi majuzi ya wawili hao haswa kwenye mitandao ya kijamii yamezua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wao ambao wamekuwa wakihoji kuhusu kinachoendelea ndani ya mahusiano yao.

Siku za hivi majuzi wapenzi hao hawajaonekana pamoja kama ilivyokuwa hapo awali ambapo walichapisha picha zao pamoja kwenye kurasa zao na hata kusifiana na kuhakikishiana kuhusu mapenzi yao kwa kila mmoja.

Kajala amekuwa akichapisha picha zake pekee yake na zingine akiwa pamoja na binti yake wa miaka 20, Paula Kajala.

"Wakati mwingine unashinda, wakati mwingine unajifunza," alisema chini ya video moja ambayo alichapisha wiki jana.

Siku chache zilizopita alichapisha picha inayoonyesha akitabasamu na kuandika," Kuwa makini, omba na usonge kimya."

Picha yake ya mwisho na Harmonize ambayo alichapisha ilikuwa mnamo Novemba 14 ambapo alikuwa akiwashukuru mashabiki wa Harmonize nchini Uganda kwa kujitokeza kwa wingi katika tamasha ambazo walifanya.

"Shukran Uganda. Kenya kuweni tayari," aliandika.

Baada ya hapo hajachapisha picha yoyote wakiwa pamoja na hata hajaonekana akimzungumzia mpenzi huyo wake.

Aidha, imebainika kuwa amebalisha bio yake ya Instagram kutoka 'mke wa @harmonize_tz' na kusalia kuwa Mama ya @therealpaulahkajala na mke na meneja.

Harmonize pia ameweza kufuata mkondo huo na kuchukua hatua ya kufuta jina Kajala Masanja kutoka kwa bio yake ya Instagram.

"Baba na mume," bio ya sasa ya staa huyo wa Bongo inasoma. 

Picha ya mwisho ya Konde Boy na Kajala kwenye ukurasa wake wa Instagram ilichapishwa mnamo Oktoba 7.

"Hakuna siku ya kupumzika @kajalafrida❤," maelezo ya picha hiyo yalisoma.

Kajala ambaye pia ndiye meneja mkuu wa Harmonize hajakuwa akitangaza wimbo wa mwisho wa mwanamuziki huyo 'Weed Language' ambao alimshirikisha staa wa dancehall kutoka Jamaica, Konshens.

Matukio haya ya hivi majuzi yamechukuliwa na baadhi ya wafuasi wao kama dokezo la matatizo kwenye mahusiano yao.