Mchungaji aliyerekodiwa akimpaka mwanamke mafuta kwenye sehemu za siri aeleza kilichojiri

Askofu Johanna amejitetea akisema kwamba alikuwa akitoa mapepo ambayo yalikuwa yamevamia ndoa ya mwanamke huyo.

Muhtasari

•Askofu Johanna alifichua kwamba ni mwanamke huyo aliyemtafuta ili amsaidie kukabiliana na masuala ya ndoa ambayo alikuwa akikabiliana nayo.

•Johanna alitumia mstari wa Biblia kuhusu uhitaji wa mgonjwa kutafuta wazee wa kanisa ili wawapake mafuta kwa ajili ya uponyaji.

Image: HISANI

Mchungaji Danson Gichuhi almaarufu Askofu Johanna hatimaye amejitokeza kufafanua kuhusu na kujitetea baada ya kupokea shutuma nyingi kutokana na video yake ‘akitoa pepo’ kutoka kwa mwanamke mmoja kwa njia  ambayo wengi wameiona kuwa chafu.

Video ambayo imekuwa ikivuma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa takriban siku mbili zilizopita inamuonyesha Askofu Johanna akipaka mafuta kwenye sehemu mbalimbali za mwili mwanamke aliyelala chali. Mtumishi huyo wa Mungu alisikika akimwombea mwanamke huyo ambaye sasa ametambulishwa kwa jina Wanjiru huku akiendelea kumpaka mafuta mwilini.

Katika mahojiano na Kururia TV, Johanna alifichua kwamba ni mwanamke huyo aliyemtafuta ili amsaidie kukabiliana na masuala ya ndoa ambayo alikuwa akikabiliana nayo.

"Video ilichukuliwa Ijumaa. Mwanamke huyo alikuwa ametoka Nairobi. Alikuja na matatizo mengi ya ndoa. Mumewe alikuwa ametoroka na kumuacha na watoto watatu. Mumewe alikuwa amechukuliwa na mwanamke mwingine. Mwanaume huyo angerudi nyumbani mchana na baadaye kwenda tena,” Askofu Johanna alisimulia

Aliongeza. “Mume wake alipoenda sana, mwanamke huyo aliona namba yangu na kunipigia. Aliniambia kuwa anataka kuja kanisani kwangu ili niweze kumhudumia. Alipokuja nilimhudumia, niliona shida alizonazo (kawaida huwa naona shida za watu). Nikamwambia kuna mwanamke anayeitwa ‘Carol’ amemchukua mumewe. Carol ndiye mwanamke aliyempokonya mume wa mwanamke huyo. Bibi huyo anaitwa Wanjiru."

Mtumishi huyo wa Mungu mwenye utata alieleza kwamba mapepo yaliyojitambulisha kama Carol ilizungumza naye na kufichua kwamba yalikuwa yameenda kwa mganga na kupakwa dawa mwili mzima ili aweze kumvutia mume wa Wanjiru.

Huku akitetea mtindo aliotumia kufukuza mapeop, Johanna alitumia mstari wa Biblia kuhusu uhitaji wa mgonjwa kutafuta wazee wa kanisa ili wawapake mafuta kwa ajili ya uponyaji.

“Kuna pepo wa kupakwa mafuta; kuna mapepo ya kuombewa. Ile ambayo mwanamke huyo alikuwa nayo ilibidi apakwe mafuta kama vile mganga alivyopaka dawa kwa mapepo. Kwa hiyo sikuvunja sheria za dini, nilifanya kulingana na mafundisho,” alisema.

Video inayomuonyesha Johanna akimwombea Wanjiru imeendelea kuzua hisia mseto kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakionekana kukosoa kitendo chake.