Mkewe Samidoh amshukuru aliyedaiwa kuwa mpango wake wa kando, Bernice kwa kumlinda mumewe

Bi Nderitu alimsifia promota huyo na kubainisha kuwa anammiss sana mumewe.

Muhtasari

•Samidoh alimshukuru promota wake Bernice Saroni kwa kuhakikisha mambo yote  yameenda sawa Marekani.

•Bernice aliweka wazi kuwa imekuwa nzuri kufanya kazi na Samidoh na kumhakikishia mke wake Edday Nderitu kwamba amekuwa salama.

Samidoh na Bernice Saroni
Image: HISANI

Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh bado yuko Ughaibuni ambako amekuwa akitumbuiza kwa wiki kadhaa zilizopita. 

Kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, amekuwa akifanya shoo Marekani ambako amepata fursa ya kukutana na mashabiki wake.

Samidoh sasa yuko nchini Uingereza ambako ameratibiwa kutumbuiza mnamo Desemba 10 kabla ya kufunga safari ya Dubai. Alimshukuru Mungu kwa kufanikisha tamasha zake zote na kuwapongeza mashabiki kwa kujitokeza.

"Mashabiki wangu, kutoka majimbo yote tofauti, Asanteni kwa kujitokeza na kuonyesha upendo mwingi. Nimenyenyekea sana.@waweru uyu, asante kwa kwenda nje ya njia yako ili kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa sawa," alisema.

Mwimbaji huyo pia alimshukuru promota wake Bernice Saroni kwa kuhakikisha mambo yote  yameenda sawa Marekani.

Bernice alibainisha kuwa ziara ya msanii huyo anayeshabikiwa sana katika eneo la Mt Kenya ilikuwa ya mafanikio.  Aliweka wazi kuwa imekuwa nzuri kufanya kazi na Samidoh na kumhakikishia mke wake Edday Nderitu kwamba amekuwa salama.

"Kila la kheri kwenye shoo za UK na Dubai. Edday Nderitu, mume wako amekuwa kwenye mikono salama, Tukutane Dubai kwenye karamu ya meli ya Desemba 17 th tufunge hii kitu ❤️🙏🙏," alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Kwa kweli, Bi Edday Nderitu alifikiwa na ujumbe wa Bernice na kufuatia hilo akatoa shukrani za dhati kwake. 

Katika ujumbe wake, Bi Nderitu  alimsifia promota huyo na kubainisha kuwa anammiss sana mume wake.

Bernice Saroni Asante sana msichana kwa kumtunza mume wangu, wewe una roho nzuri sana, asante Mungu safari ilifanikiwa, Siwezi kungoja kumuona tunammiss sana, tuonane Dubai mnamo tarehe 17 mpenzi❤️," alisema chini ya chapisho la Bernice.

Mwezi uliopita Samidoh aliibuka kuwa gumzo mitandaonihuku akidaiwa kuwa na uhusiano ya kimapenzi na promota wake Bernice Saroni.

Huku tetesi za mahusiano zikiendelea, mwimbaji huyo hakujitokeza kuthibitisha au kukanusha madai hayo. Badala yake aliendelea kuwachanganya wanamitandao kuhusu uhusiano wake promota huyo.

Katikati mwa mwezi jana, mwanamuziki huyo alichapisha video iliyomuonyesha akifurahia muda mzuri na Bernice. Katika video hiyo, wawili hao walijawa na tabasamu usoni huku wakiimba wimbo wa Kikuyu  pamoja.

Kama kawaida, wanamitandao walimiminika chini ya chapisho hilo na kutoa maoni tofauti kuhusu video hiyo.

"Heshimu mama watoto kaka," mtumizi mmoja wa Tiktok alimwambia mwimbaji huyo.

Samidoh alijibu, " Toa maoni kuhusu mambo ambayo unaelewa kaka. Vinginevyo, hiyo kiherehere pelekea bibi yako."

Staa huyo wa Mugithi pia aliwasuta wanamitandao wengine ambao walijaribu kumvuta Bernice kwenye ndoa yake na kudai kuwa alichapisha picha zake ili kumuumiza mkewe.  Baadhi ya wanamitandao hata hivyo waliibua madai kuwa mwanadada huyo ni mwanafamilia wa Samidoh na kusema wanajua walichokuwa wakifanya.

Mzazi mwenza wa Samidoh, Karen Nyamu pia alidaiwa kuzozana na Bernice kuhusu mwimbaji huyo.

Karen alipoulizwa ikiwa anapigania mzazi huyo mwenzake alisema, ""Simpiganii, lakini anastahili kupiganiwa,"