Ndoa sio kuwa mwaminifu, kucheat sio msingi wa kumuacha mtu- Bien azungumzia ndoa yake

Bien alisisitiza kuwa wapenzi hawapaswi kuwa wafungwa katika ndoa wala kumilikiana.

Muhtasari

•Bien na Kuruka wamekuwa pamoja kwa miaka minane na walifunga pingu za maisha takriban miaka mitatu iliyopita.

•Kulingana na Bien, kucheza karata nje ya ndoa sio suala lenye uzito mkubwa  kiasi cha kutenganisha wanandoa.

Bien na mke wake Chiki Kuruka
Image: INSTAGRAM// CHIKI KURUKA

Mwanabendi wa Sauti Sol Bien-Aime Baraza amekana madai ya kuwa kwenye ndoa ya wazi na mke wake Chiki Kuruka.

Wanandoa hao wamekuwa pamoja kwa miaka minane na walifunga pingu za maisha takriban miaka mitatu iliyopita.

Kwa muda mrefu imekuwa ikidaiwa kuwa Bien aliwahi kusema kuwa yeye na mkewe wote wako huru kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu yeyote wa nje wanayevutiwa naye licha ya kuwa kwenye ndoa, madai ambayo amefutilia mbali kwa sasa.

"Sipo kwenye ndoa ya wazi. Natamani ningekuwa. Sikusema nipo kwenye ndoa ya wazi, watu hupenda kujijazia. Kuna chenye huwa unasema na kuna chenye watu husikia," Bien alisema katika mahojiano na Eve Mungai.

Mwimbaji huyo hata hivyo alisisitiza kuwa wapenzi hawapaswi kuwa wafungwa katika ndoa na hawapaswi kumilikiana.

"Katika ndoa, hutakiwi kumiliki mwenza wako, unatakiwa kupata na uzoefu na mpenzi wako. Ndoa si mambo na kuwa mwaminifu sana na mpenzi wako. Ndoa ni kuhusu kutembea safari ya maisha pamoja," Alisema.

Kulingana na msanii huyo wa Sauti Sol, kucheza karata nje ya ndoa sio suala lenye uzito mkubwa  kiasi cha kuivunja. 

Bien alidokeza kuwa anaweza kumsamehe mke wake ikitokea ateleze na kuwa na mahusiano nje ya ndoa.

"Kuna vitu vingi ambavyo unajenga na mke wako ambavyo ni zaidi hisia za wivu katika mahusiano yako. Sidhani kucheat ni msingi wa kuachia mtu. Kuna mambo mabaya zaidi ambayo mtu anaweza kukufanyia," Alisema Bien.

Mwanamuziki huyo pia alidai kuwa wanandoa hawapaswi kubadilishana nambari za siri za kufungua simu zao.

Alibainisha kuwa anamwamini mpenzi wake na kwa hiyo hakuna haja ya yeye kumchunguza kwa simu

"Nenosiri sio ya kukulinda kutoka kwa mwenzi wako,ni ya kukulinda kutoka kwa watu wenye nia mbaya," Alisema.

Bien pia aliwashauri wanandoa kuangazia ndoa zao zenyewe bila kuzilinganisha na ndoa za watu wengine.