"Next time ni yeye asijam!" Karen Nyamu ajibu baada ya Samidoh kukana alimnunulia pombe ya 420,000

"Mwambie next time ni yeye asijam. Hata hakuna mahali nilimtaja. Niko na baba na baby daddy wawili," Karen Nyamu alisema.

Muhtasari

•Samidoh alibainisha kwamba katika video yake hakuwahi kufafanua ni mwanaume yupi katika maisha yake ambaye alimnunulia pombe hiyo ya takriban shilingi nusu milioni.

•Samidoh alidokeza kuwa mzazi huyo mwenzake alidanganya kuhusu kumnunulia pombe ya bei ghali.

Karen Nyamu na Samidoh
Image: HISANI

Seneta Karen Nyamu hatimaye amemjibu mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh baada ya kukana hadharani kupokea zawadi ya pombe ya bei ghali yenye thamani ya shlingi 420,000 kutoka kwake Siku ya kuwasherehekea kina Baba mwezi uliopita.

Siku ya Jumatatu, Samidoh ambaye ana watoto wawili na mwanasiasa huyo alidokeza kuwa mzazi huyo mwenzake alidanganya kuhusu kumnunulia pombe ya bei ghali.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, mwimbaji huyo wa Mugithi aliweka wazi kwamba zawadi hiyo haikuwa yakweli na ilikuwa ni maigizo tu.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook siku ya Jumapili jioni, aliandika, “Waweru Uyu na Kajei Salim kumbe maswali zenu nyingi za kifala ni za Captain Morgan. Kwa sababu bia haiulizi maswali ya kipuuzi buana. Niko Muthiga kujeni mnipige.”

Mwimbaji huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa ameshikilia kikombe ambacho kilionekana kuwa na pombe ndani yake.

Mmoja wa mashabiki wake alitaka kujua iwapo pombe aliyokuwa ameshika ni ile ambayo Karen Nyamu alidaiwa kumnunulia.

“Thamweri, hiyo ni ile ya 420k. Bado iko kwa friji,” Princess Priscah Wambui alitoa maoni chini ya chapisho la mwimbaji huyo.

Katika jibu lake, Samidoh aliwataka wanamitandao kutochukulia kila kitu kwa uzito akidokeza kwamba pombe ya bei ghali inayodaiwa alinunuliwa na mzazi mwenzake si ya kweli.

“Hehe hizo ni vipindiree vya mitandao ya kijamii usichukulie serious sana. Naweza rogwa bure,” alijibu.

Kufuatia ufichuzi wa mwimbaji huyo, baadhi ya wanamitandao walikimbilia katika kurasa za mitandao ya kijamii za Karen Nyamu kumdhihaki kuhusu kile ambacho baba ya watoto wake wawili wadogo alisema.

"Samidoh ameruka ile story ya gift ya father's day kipetero," mtumiaji wa Instagram kendyreborn aliandika kwenye moja ya machapisho ya seneta huyo.

Katika jibu lake, mama huyo wa watoto watatu alibainisha kwamba katika video yake hakuwahi kufafanua ni mwanaume yupi katika maisha yake ambaye alimnunulia pombe hiyo ya takriban shilingi nusu milioni.

Karen Nyamu alikuwa na ujumbe wa wazi kwa waliodhani alimaanisha Samidoh wakati aliposema anamnunulia zawadi ‘mubaba’ wake huku akibainisha kuwa ana baba mzazi na wazazi wenza wawili.

"Mwambie next time ni yeye asijam. Hata hakuna mahali nilimtaja. I have a dad and two baby daddies," Karen Nyamu alisema.

Kumaanisha, "Mwambie wakati mwingine ni yeye asikasirike. Hata hakuna mahali nilimtaja. Nina baba na baba watoto wawili."