"Ningekuwa nimemaliza kujenga!" Akothee afichua mamilioni aliyotumia kumsomesha bintiye chuo kikuu

Mwimbaji huyo amesema Makadia amekuwa akilipa karo mwenyewe baada ya kuzituma kwenye akaunti yake.

Muhtasari

•Akothee alifichua kuwa Makadia amekuwa akijilipia karo ya chuo kikuu baada yake kuzituma kwenye akaunti yake.

•Akothee amefichua kuwa masomo ya Makadia yamekuwa yakimgharimu takriban shilingi milioni 3.8 kila mwaka.

Image: INSTAGRAM// FANCY MAKADIA

Mwimbaji mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amemsherehea bintiye mdogo Fancy Makadia kwa kukamilisha masomo yake ya chuo kikuu.

Akothee ambaye kwa sasa yuko Ulaya alichukua hatua hiyo baada ya kukutana na Makadia akienda kuhudhuria mahojiano ya kazi  jijini Paris, Ufaransa.

Amesema kuwa  mtoto huyo wake wa tatu amekuwa akiishi pekee yake tangu alipohamia Ufaransa akiwa na miaka 17. Alisema Makadia amekuwa akijilipia karo ya chuo kikuu baada yake kuzituma kwa akaunti yake.

"Sijawahi kulipa karo moja kwa moja shuleni. Nilituma pesa  kwenye Akaunti yake, kwa hivyo alikuwa na chaguo la kununua maisha yake ya baadaye au kutumia pesa na kuanza kulaumu kila mtu," Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto watano amefichua kuwa masomo ya Makadia yamekuwa yakimgharimu takriban shilingi milioni 3.8 kila mwaka.

Hii inamaanisha mwanamuziki huyo ametumia zaidi ya shilingi milioni 15 kwa masomo ya chuo kikuu ya Makadia.

"Ningekuwa nimemaliza kujenga lakini nimejenga mtu," Alisema.

Amedai kwamba hakuna mtu yeyote aliyemsaidia kulipa karo ya bintiye katika kipindi cha miaka minne ambacho amekuwa akisoma Ufaransa.

Licha ya kupata shahada yake ya kwanza, Makadia tayari amemfahamisha mamake kuwa anatazamia kuendeleza masomo yake huku akifanya kazi.

Kufuatia mafanikio hayo, Akothee amempongeza binti huyo wake na kueleza jinsi alivyomfanya kujivunia.

"Hongera sana mtoto wangu @fancy_makadi. Umenifanya nijivunie. Nakupenda sana malkia," Akothee alimwambia bintiye.

Kufikia sasa mabinti wote watatu wa Akothee tayari wamekamilisha masomo yao ya chuo kikuu na kupata shahada ya kwanza.

Binti wa kwanza wa msanii huyo, Vesha Okello alihitimu kutoka chuo kikuu cha Strathmore mwezi Desemba 2020.

Rue Baby ambaye ni mtoto wa pili wa Akothee alihitimu kutoka chuo hicho hicho Desemba mwaka jana.

Watoto wawili wa mwisho wa mwanamuziki huyo wanasomea Ufaransa ambako wanaishi na baba mtoto wake wa mwisho.