Mamangu alinipeleka polisi baada ya kutoroka ili kuolewa nikiwa na miaka 14- Akothee afunguka

Amekiri kuwa bado anaogopa kuwatambulisha wapenzi wake wapya kwa mamake kutokana na ukali wake.

Muhtasari

•Akothee alifichua zaidi kuwa mamake hakupenda familia ambayo alitoroka kwenda kuolewa, ndiposa alimshinikiza sana arudi shuleni.

•Amefichua kuwa mama yake ndiye aliyempatia dawa yake ya kwanza ya kupanga uzazi baada ya kujifungua bintiye wa kwanza.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amefichua kuwa alitoroka nyumbani kwao na kuenda kuolewa akiwa na umri mdogo wa miaka 14 tu.

Mama huyo wa watoto watano amekiri kwamba hatua hiyo kwa kweli ilivunja moyo wa mzazi huyo wake kwani alikuwa na matumaini makubwa naye.

"Nilikuwa binti yake wa Kwanza kuzaliwa mwenye maarifa. ✌️Nilikuwa mtoto muasi. Wanafunzi wenzangu kutoka Nyabisawa Girls wanaweza kukuambia, nilipenda kucheza densi na nilijibandika jina dada wa Yondo," Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 alisema kuwa mapenzi yake kwa muziki na dansi yalipiku mengine yote lakini mamake alitia juhudi  kumchunga na kumlea kulingana na maadili ya Kikristo.

Alifichua kuwa mzazi huyo wake ambaye kitaaluma ni mwalimu hata alichukua hatua ya kumpeleka katika vituo kadhaa vya polisi baada ya kukatisha masomo yake ili aolewe akiwa na umri mdogo sana.

"Mama yangu alikuwa na matumaini makubwa sana kwangu, nilimtia machozi, nilimdhalilisha sana, nilimkatisha tamaa sana, alinipeleka katika vituo kadhaa vya polisi ili tu nirudi shuleni, dawa ya kwanza ya kupanga uzazi niliyotumia ni vidonge, nilipewa na mama yangu baada ya kujifungua Vesha," Alisema.

Akothee alifichua zaidi kuwa mamake hakupenda familia ambayo alitoroka kwenda kuolewa, ndiposa alimshinikiza sana arudi shuleni.

"Alinirudisha shuleni Asego kanyada, Akoth aliacha shule tena baada ya Kidato cha kwanza,"

Hadi kufikia sasa msanii huyo bado anaogopa kuwatambulisha wapenzi wake wapya kwa mamake kutokana na ukali wake

Amesema mzazi huyo wake anamtambua tu aliyekuwa mumewe wa kwanza na ambaye ni baba ya mabinti wake watatu, Jared Okello .

Hapo awali aliwahi kufichua kuwa mama yake sasa ana upendo mkubwa sana kwa mume huyo wake wa zamani.

"Weeee niseme nini tena baada ya Mungu kupatia mama wa ajabu kwa mwanamke mzuri kama mimi‼️ Ash mapenzi mama yangu anayo kwa Ex wangu, naapa kama angekuwa na uwezo wa kuniweka hapa kwa nguvu, angeyasikiliza maneno yake yenye nguvu," Akothee alisema wakati akimuomboleza babake Jared mwezi Mei.

Licha ya kusambaratika kwa ndoa yake na Jared, Mamake Akothee alimshinikiza kununua kipande cha shamba na kujenga karibu na wakwe hao wake.