"Nitakumiss!" Gidi na bintiye wajawa na huzuni huku wakiagana kwaheri (+video)

Marie-Rose aliweka sura inayoonyesha kwamba hakutaka babake aondoke.

Muhtasari

•Gidi alitumia likizo yake kutembelea familia yake nchini Ufaransa na kuwa na wakati mzuri na binti yake mdogo Marie-Rose.

•Mtangazaji huyo alipomuuliza bintiye ujumbe wa mwisho kwake kabla ya kuondoka, Marie-Rose alijibu, "Nitakumiss."

Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi anatazamiwa kurejea kazini hivi karibuni i baada ya kuwa kwenye likizo fupi.

Gidi alitumia likizo yake kutembelea familia yake nchini Ufaransa na kuwa na wakati mzuri na binti yake mdogo Marie-Rose ambaye bila shaka ana uhusiano wa karibu sana naye.

Mtangazaji huyo mahiri na bintiye walitengeneza kumbukumbu nzuri pamoja wakati wa kikao chake cha muda mfupi na alipokuwa akijiandaa kurejea Kenya, kwaheri yao haikuwa rahisi na iligeuka kwa kipindi cha kihisia kama alivyoonyesha Gidi kwenye video.

"Kwaheri sio rahisi😫," Gigi aliandika chini ya klipu fupi ya video aliyochapisha Instagram akimfahamisha bintiye kuwa anarudi Kenya na kumuaga kwaheri.

Kwenye video hiyo, Marie-Rose anaonekana akiwezwa na hisia pindi tu baada ya baba yake kumuarifu kwamba anataka kuondoka ili kurudi nchini Kenya.

"Marie-Rose, narudi Kenya," Gidi anasikika akimwambia bintiye.

Punde baada ya kusema hayo, binti yake alijibu kwa 'Hapanaa' kubwa na kuweka sura ya uso inayoonyesha kwamba hakutaka aondoke.

Mtangazaji huyo alipomuuliza bintiye ujumbe wa mwisho kwake kabla ya kuondoka, Marie-Rose alijibu, "Nitakumiss."

Pia alimhakikishia malkia huyo mdogo kwamba atamkosa sana pia baada ya kuondoka. Wawili hao kisha wanaonekana wakikumbatiana kihisia.

Gidi aliungana na familia yake iliyo Ufaransa mwishoni mwa mwaka jana na amekuwa akifurahia muda na bintiye kwa siku kadhaa.

"Wakati msichana huyu mdogo (Marie-Rose) amefurahi, tunafurahi. Heri ya mwaka mpya mapema kutoka kwa Marie-Rose,"  alisema wiki jana kupitia Instagram baada ya kutua katika nchi hiyo ya Ulaya.

Imekuwa mazoea ya mtangazaji wa kipindi cha asubuhi kumtembelea bintiye mara kwa mara wakati anapochukua mapumziko kutoka kazini.