Gidi aahidi kusaidia kuboresha alikokuwa akiishi Dandora baada ya kufanya ziara (+picha)

Wakazi wa Dandora walimueleza Gidi matatizo yanayowakumba na akahidi kufuatilia.

Muhtasari

•Gidi alitumia ziara yake kutembelea shule ya msingi aliyosomea, nyumba yake ya zamani ya kukodisha na pia kutangamana na baadhi ya marafiki wake wa zamani.

•Baadhi ya mashabiki ambao alitangamana nao walisikika wakiuliza alikomwacha mtangazaji mwenzake Ghost Mulee.

Image: INSTAGRAM/// GIDI OGIDI

Siku ya Jumapili mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo Joseph Ogidi almaarufu Gidi alizuru mtaa wake wa kuzaliwa wa Dandora, jijini Nairobi.

Gidi alitumia ziara yake kutembelea shule ya msingi aliyosomea, nyumba yake ya zamani ya kukodisha na pia kutangamana na baadhi ya marafiki wake wa zamani.

Wakazi wa Dandora walitumia fursa hiyo kueleza baadhi ya matatizo yanayokumba eneo hilo na baada ya kuwasikiliza mtangazaji huyo mahiri akahidi kufuatilia.

"Ilikuwa ni nyakati za kihisia kutembelea mtaa nilikozaliwa na kukulia DANDORA PHASE 4. Ahsante sana watu wa D kwa makaribisho. Kwa vijana, nimesikia kero zenu nitatumia ushawishi wangu kuboresha mtaa wetu," Gidi alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliahidi kuanza kwa kuzungumza na gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ili kufungua uwanja wa Dandora hivi karibuni ili vijana wa eneo hilo wapate mahali pazuri pa kufanyia mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali.

Mtangazaji wa kipindi cha asubuhi alifurahi kutembelea iliyokuwa shule yake ya msingi na kuyaona baadhi ya madarasa ambayo alisomea. Pia alipata fursa ya kukutana na mwalimu mkuu wa sasa wa shule hiyo.

Katika moja ya video alizochapisha, Gidi alionekana akionyeshana nyumba ambayo alikuwa akiishi zamani katika mtaa huo.

"Hii ndiyo nyumba ya kwanza niliyoishi nilipokuja Nairobi. Hapa ndipo nilipoishi, ni nyumba ya vyumba viwili," alisema. 

Pia alionyesha eneo la burudani alilopenda kutembelea wakati alipokuwa akiishi pale.

Tazama picha za Gidi akitangamana na mashabiki wake mtaani Dandora Phase IV  chini hapa:-

Baadhi ya mashabiki ambao alitangamana nao walisikika wakiuliza alikomwacha mtangazaji mwenzake Ghost Mulee.

"Ghost yuko.. nashukuru" alimjibu shabiki mmoja aliyeeleza upendo wake kwa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi.

Gidi alizaliwa na kukulia katika mtaa wa Dandora kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Aquinas kisha kuendeleza masomo yake katika vyuo kikuu cha JKUAT na KCA.

Kabla ya kujiunga na Radio, Gidi alifanya kazi katika Umoja wa Mataifa na pia alikuwa mwanamuziki. Alikuwa kwenye kundi la Gidi Gidi Maji Maji.