Otile Brown afunguka kuhusu kipusa anayemezea mate

Brown amemtambua Braxton kama kiumbe maalum cha Mungu.

Muhtasari

•Otile Brown amekiri kuwa anammezea mate sana mwimbaji wa R&B Toni Braxton.

•Braxton ni mmoja wa wasanii wa R&B wanaoshabikiwa sana kote ulimwenguni.

Image: INSTAGRAM// OTILE BROWN

Mwimbaji mashuhuri wa Kenya Jacob Obunga almaarufu Otile Brown amefichua mwanadada anayemkubali zaidi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Brown amekiri kuwa anammezea mate sana mwimbaji wa R&B Toni Braxton.

Mpenzi huyo wa zamani wa mwanasoshalaiti Vera Sidika amemtambua Braxton kama kiumbe maalum cha Mungu.

"Bado namcrushia.. Mmoja wa wanawake wazuri zaidi ambao Mungu aliwahi kuumba," Brown aliandika.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha ya kusisimua macho ya mwimbaji huyo maarufu kutoka Marekani.

Braxton ni mmoja wa wasanii wa R&B wanaoshabikiwa sana kote ulimwenguni. Kwa mujibu wa Wikipedia, malkia huyo wa muziki amewahi kuuza zaidi ya rekodi milioni 70 za muziki wake.

"Braxton amewahi kushinda Tuzo saba za Grammy, Tuzo tisa za Muziki za Billboard, Tuzo saba za Muziki za Marekani, na tuzo zingine nyingi," Wasifu wake katika Wikipedia unasema.

Kando na muziki, mzaliwa huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 54 pia ni mjasiriamali na anamiliki kampuni ya vipondozi.

Aliwahi kuwa kwa ndoa na Keri Lewis kwa kipindi cha takrina mwongo mmoja na walibarikiwa na watoto wawili pamoja.

Otile Brown amefunguka hisia zake kuhusu Braxton takriban miezi mitano baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake Nabayet.

Mwezi Januari mwanamuziki huyo alitangaza kwamba yeye na Nabbi walitengana kwa njia ya makubaliano.

"Mimi na Nabbi hatuko pamoja tena. Mara ya mwisho tulikuwa pamoja ilikuwa kujaribu kutafuta njia ya mbele lakini tuliamua kwenda tofauti kwa bahati mbaya," Brown alitangaza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Licha ya kutengana kwao, Brown alieleza kwamba yeye na malkia huyo kutoka Ethiopia wangeendeleza uhusiano mzuri.