"Tafadhali nisamehe!" Jimal Rohosafi ajuta kuharibu ndoa yake, aomba msamaha kwa mkewe

Ndoa yake ilianza kuporomoka baada ya kujitosa kwenye mahusiano na mwanasoshalaiti Amber Ray

Muhtasari

•Jamal amekiri kuwa alimkosea sana mama huyo wa watoto wake wawili kwa kuingiza drama nyingi kwenye ndoa yao.

•Amedokeza kuwa yupo tayari kupiga hatua zozote ili kufufua ndoa yao iliyokufa miezi kadhaa iliyopita.

Jimal Rohosafi na mkewe Amira
Image: INSTAGRAM

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki Matatu jijini Nairobi Jamal Marlow Rohosafi amejitokeza kumuomba msamaha mkewe Amira.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jamal amekiri kuwa alimkosea sana mama huyo wa watoto wake wawili kwa kuingiza drama nyingi kwenye ndoa yao ya miaka mingi.

"Naomba radhi kwa kukukosea heshima, kukuaibisha, kwa kukuumiza, kwa maumivu yote na kwa huzuni niliyokuletea. 💔Samahani kwa nyakati zote ambazo sijawa mwanaume niliyeahidi kuwa," Jamal alimuandikia mkewe.

Mfanyibiashara huyo amekiri kuwa alikosa kutimiza  wajibu wake wa kumlinda mkewe kama alivyohitajika kufanya.

Amesema kwamba alifahamu wakati ndoa yake ikiporomoka ila akashindwa na la kufanya kwa wakati ule.

"Ilikuwa mbaya kabisa. Huenda nilionekana kama mtu asiye na wasiwasi lakini sikuwa na la kufanya. Nilijua haikuwa sawa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya!Amira nafanya hivi kwa sababu ukosefu wa heshima pia ulikuwa mkubwa. Naomba radhi kwa kukosa heshima," Aliandika.

Jamal pia amekiri kwamba hajakuwa sawa tangu alipokosana na mke huyo wake na mama ya watoto wake.

Amedokeza kuwa yupo tayari kupiga hatua zozote ili kufufua ndoa yao iliyokufa miezi kadhaa iliyopita.

"Tafadhali nisamehe. Mimi na wewe tumetoka mbali na kukupitishia kwa yote hayo hakukuwa kuzuri. Tafadhali nisamehe Amira," 

Ndoa ya Jamal ilianza kuzama mwaka jana baada yake kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na mwanasoshalaiti Amber Ray.

Mfanyibiashara huyo alikumbwa na mkanganyiko kuhusu amchague nani wakati wapenzi wake wawili walipoanza kupigana.

Baadae aliamua kumchagua Amber Ray, jambo ambalo lilimkera Amira ambaye mwezi Novemba alianza mikakati ya talaka. 

"Kutoka leo tafadhali mnichukulie kama single mum. @jimal_rohosafi tayarisha karatasi ya talaka. Sitakubali unikosee heshima tena!!" Amira alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram takriban miezi tisa iliyopita.

Wakati huo alitangaza kuwa angezingatia kulea watoto na kuendeleza biashara yake huku akilenga kusonga mbele na maisha yake.

Mahusiano ya Jamal na Amber Ray hata hivyo hayakudumu kwani walitengana baada ya mwishoni mwa mwaka jana.

Amber Ray amekuwa kwa takriban mahusiano mengine matatu baada ya kutengana na mfanyibiashara huyo.