"Tunajiangusha na mila zilizopitwa na wakati!" Nameless ajibu shinikizo la kupata mtoto wa kiume

Mwanamuziki Nameless na mke wake Wahu ni wazazi wa mabinti watatu warembo.

Muhtasari

•Nameless alidokeza kuwa angependa kukumbukwa kama baba ya wasichana wazuri waliojawa na hekima, wanyenyekevu na wenye upendo.

•Mwimbaji huyo sasa amewataka watu kukumbatia mabadiliko ya kitamaduni ili kuweza kusonga mbele na wakati.

Wahu// Nameless
Image: INSTAGRAM// NAMELESS

MwanamuzikiDavid  Mathenge almaarufu Nameless amekosoa baadhi ya tamaduni za jamii ambazo baadhi ya Wakenya bado wanazitilia maanani.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, baba huyo wa mabinti watatu amebainisha kuwa baadhi ya mila zimepitwa na wakati na kuwataka watu kutumia busara ili kubaini zile ambazo si za haki na zisizo na maendeleo.

"Ninaelewa kuwa tumefundishwa kufuata tamaduni au mila zetu bila maswali, lakini ukweli ni kwamba tunapaswa kutumia busara kubaini sehemu za tamaduni zetu ambazo sio za haki au zisizo na maendeleo na kuziacha ziende, tunapoendelea zaidi. njia za haki na bora za kufikiri na kuishi," alisema.

Mume huyo wa Wahu Kagwi alikuwa akiwajibu  baadhi ya wanamitandao ambao wamekuwa wakimpa shinikizo la kupata mtoto wa kiume.

Nameless na mke wake Wahu ni wazazi wa mabinti watatu warembo; Tumiso Mathenge ambaye ni mzaliwa wa kwanza, Nyakio Mathenge na Wanjiru Mathenge ambaye alizaliwa siku chache tu ambazo zimepita.

"Tafuta kijana boss.. uridhi wako, sisi ni Waafrika," mtumizi mmoja wa Facebook alimwaambia Nameless chini ya moja ya machapisho yake.

Mwimbaji huyo ambaye alionekana kutoridhishwa na ujumbe wa mwanamitandao huyo alibainisha kuwa ameridhika kujaliwa mabinti pekee.

Katika jibu lake alidokeza kuwa angependa kukumbukwa kama baba ya wasichana wazuri waliojawa na hekima, wanyenyekevu na wenye upendo.

"Ninataka kuwa baba wa wasichana watatu warembo ambao wataishi maisha ya kuwajibika ambayo yanaunda amani na furaha kwao na wengine karibu nao. Kwao, hayo ndiyo maono ninayofanyia kazi," alisema.

Nameless amekuwa akipokea shinikizo kubwa la kupata mtoto wa kiume kuona kwamba tayari ana mabinti watatu sasa.

Mwimbaji huyo sasa amewataka watu kukumbatia mabadiliko ya kitamaduni ili kuweza kusonga mbele na wakati.

“Jamani, msifuate tamaduni tu bila kuuliza maswali na kuangazia njia bora za kuishi pamoja kama watu. Hebu tuendeleze buana” alisema.

Nameless alitangaza kuzaliwa kwa mtoto wake wa tatu mapema wiki hii na kumpatia jina la dada yake mkubwa, Shiru.