Baba mabinti: Nameless amsifia bintiye kifungua mimba, asema yuko tayari kuwalea dada wadogo

Nameless na Wahu wanatarajia mtoto wao wa tatu ambaye pia ni wa kike kujiunga na mabinti wengine wawili.

Muhtasari

• BabaGalzChairMan! Nimeheshimiwa, Nimebarikiwe na kujawa na furaha kochokocho - Nameless.

Nameless amsifia bintiye kifungua mimba
Nameless amsifia bintiye kifungua mimba
Image: Instagram

Msanii mkongwe kwenye Sanaa ya muziki wa kizazi kipya nchini Kenya, Nameless baada ya kuweka wazi jinsia ya mwanawe mtarajiwa, sasa rasmi ameanza kujiita baba mabinti.

Mwishoni mwa wiki jana, Nameless na mkewe Wahu Kagwi walifanya tafrija ya kufichua jinsia ya kijacho wao ambaye pia ilifahamika ni mtoto wa kike, kufikisha mabinti watatu katika familia ya Mathenge, kama wanavyojiita jina la ukoo.

Baba Wasichana Jumamosi amepakia msururu wa picha akiwa na mabinti wake wawili huku akisema kuwa binti wake mkubwa sasa yuko tayari kabisa kuwaongoza wenzake wawili akiwemo huyo mmoja ambaye anatarajiwa hivi karibuni.

Nameless anajiita mwenyekiti wa chama cha baba mabinti na kundi la kulea watoto wa kike, na ameonesha Imani yake kubwa kwa binti yake kifungua mimba kwa jina Tumiso na kusema kuwa amejiweka tayari kabisa kuwaongoza dada zake wadogo.

“BabaGalzChairMan! Nimeheshimiwa, Nimebarikiwe na kujawa na furaha kochokocho. Binti wa mfalme ambaye ni wa kwanza kabisa Tumiso anatarajia kuwaongoza dada zake kwa mfano 🙏🏿💚💚💚 na tayari anamfanya Baba kuwa kujihisi wa kujivunia!” Nameless aliandika huku akiwashukuru wote waliowahongera wakati wa kuweka wazi jinsia ya mtoto wao mtarajiwa.

Wanandoa hao wanaopigiwa upato kuwa wanandoa wenye umaarufu na ambao wamefanikiwa kudumu pamoja kwa miaka 20 na ushee walisherehekea kuadhimisha miaka 17 tangu harusi yao mwezi mmoja uliopota.

Wahu na Nameless walikula yamini ya kuishi pamoja kama mke na mume mbele ya hadhira ya waumini mnamo Septemba 10 mwaka 2005 na mwezi jana tarehe kama hiyo walisherehekea kwa kupakia video ya jinsi matukio yalivyokuwa miaka 17 iliyopita.

Kando na kuwa kweney ndoa kwa miaka 17, wawili hao wamekuwa kwa mahusiano kwa miaka 25 jumla na ile minane waliyochumbiana.

Hongera kwao!