Nameless ashukuru Mungu kwa ndoa yake ya miaka 17 huku wakitarajia mtoto wa 3

Nameless na Wahu hivi karibuni wanasubiria kumpokea mtoto wa tatu majaaliwa

Muhtasari

• Mwezi mmoja uliopita wanandoa hao walisherehekea miaka 17 ya kudumu katika ndoa tangu kuvishana pete za harusi mwaka 2005.

Nameless na Wahu
Nameless na Wahu
Image: Instagram

Mwanamuziki mkongwe wa kizazi kipya nchini Kenya Nameless amepakia picha moja maridadi wakiwa na mke wake mjamzito Wahu.

Katika picha hiyo, Nameless amemshukuru Mungu kwa kuwagandisha pamoja kama ruba kwa zaidi ya miaka 15 ya ndoa na jumla ya zaidi ya miongo miwili ya mahusiano.

“Familia ya kina Mathenge, ahsante Mungu kwa kutufikisha hatua hii katika maisha yetu,” Nameless aliandika huku akiwa amemkumbatia mkewe Wahu.

Mwezi mmoja uliopita wanandoa hao walisherehekea miaka 17 ya kudumu katika ndoa tangu kuvishana pete za harusi mwaka 2005.

Katika video hiyo ambayo Wahu aliipakia  siku hiyo, ilionesha jinsi harusi yao ya kiasili ilifanyika na Nameless pia alimshukuru Mungu kwa kuwaweka pamoja muda huo wote.

Pia alifunguka kuwa hata kama ndoa yao imedumu kwa miaka 17, mahusiano yalianza miaka 25 iliyopita.

Wahu alirusha dongo kwa jarida moja la humu nchini ambalo alisema kipindi hicho lilikuwa maarufu sana. Jarida hilo kulingana na Wahu lilitabiri kuwa mahusiano yao hayangedumu zaidi ya miaka 2 na siku ya kusherehekea miaka 17, aliwapiga mafamba waandishi wa jarida hilo kuwa utabiri wao ulikunywa maji.

Nameless na Wahu hivi karibuni wanasubiria kumpokea mtoto wa tatu majaaliwa. Kwa sasa ni wazazi wa mabinti wawili.